Rais Shein awasamehe wafungwa 12

Friday January 11 2019

 

By Muhammed Khamis, Mwananchi [email protected]

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ametoa msamaha kwa wanafunzi 12 ambao walikuwa wakiendelea kutumikia vyuo vya mafunzo Unguja na Pemba.

Wanafunzi hao ni wafungwa ambao kwa Zanzibar wanachukuliwa kuwa wako katika mafunzo ya kuwa raia wema baada ya vifungo vyao.

Dk Shein ametoa msamaha huo ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar zitakazofanyika kesho, Jumamosi, Januari 12, 2019.

Kwa Tanzania Bara, wanafunzi ni wafungwa na vyuo vya mafunzo ni magereza.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa SMZ ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Abdulhamid Yahya Mzee imesema kwa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar 1984, Rais Shein ameamuru kifungo kilichobaki cha wanafunzi walionufaika na msamaha huo ambao walikuwa wanaendelea kutumikia kifutwe na waachiwe huru kuanzia leo Alhamisi.

Amesema kwa kuwa Zanzibar itakuwa inasherehekea miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar kesho na Rais ameridhika kuna sababu za kutosha za kutumia uwezo wake huo katika sherehe hiyo, wanafunzi hao waachiwe.

Walionufaika na msamaha huo kwa Unguja ni Mushtaki Mustafa Hashim, Ramadhan Abubakar Jabu, Bakari Khamis Juma, Maulid Kheir Suleiman, Othman Ramadhan Shija, Faiz Juma Faiz na Ali Haji Ali.

Kwa upande wa Pemba ni Suleiman Ali Suleiman, Ali Omar Ali, Ibrahim Mbarouk Omar, Mohamed Othman Ali na Mbarouk Ali Mbarouk.

Msamaha huo ambao hutolewa kila mwaka katika kipindi cha sherehe za Mapinduzi huhusisha wanafunzi ambao ni wazee sana, wenye maradhi sugu au makosa madogo ambao wamebakiza muda mfupi wa kutumikia vyuoni, wanaoonyesha nidhamu nzuri na kujutia makosa yao.

Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo, wenye makosa mauaji kwa makusudi, wizi wa kutumia nguvu, wizi wa mali ya umma, udhalilishaji wa wanawake na watoto, dawa za kulevya na wenye makosa mengi ya zamani kwa kawaida huwa hawapewi msamaha.


Advertisement