Rais akemea nyimbo, matangazo ya kumsifia

Muktasari:

Rais huyo ametaka vyombo vya habari kujikita zaidi katika kutangaza mafanikio ya nchi, kazi kubwa inayofanywa na wananchi bila ya kuchoka na uzuri wa taifa hilo la kale.

 

 


Kiongozi wa Tajikistan ametaka kukomeshwa kwa nyimbo zinazomsifu, televisheni ya serikali imetangaza leo, katika kipindi ambacho sifa kwa kiongozi huyo zinazidi kuongezeka.

Kiongozi shupavu wa muda mrefu, Emomali Rakhmon ameeleza kutofurahishwa na matangazo yaliyozidi kiasi ya kumsifu kwa kutumia video za muziki, kituo hicho kilisema.

"Badala yake, rais ameagiza uongozi wa Kamati ya Televisheni na Matangazo ya Redio kujikita zaidi kutangaza habari za wananchi wanaofanya kazi bila ya kuchoka, mafanikio makubwa ya nchi na uasili wa taifa hilo la kale," televisheni hiyo ilisema.

tabia ya kumsifu rais ni ya kawaida katika nchi hiyo ya barani Asia ambayo ilikuwa chini ya utawala wa Russia na ambayo viongozi wake hupata upinzani mdogo wa kisiasa na hauna vyombo huru vya habari.

Katika nchi jirani ya Uzbekistan, mamlaka pia zimeonya dhidi ya muziki unaomwaka sifa kwa Rais Shavkat Mirziyoyev.

Taasisi ya ikulu inayoshughulika na uratibu wa muziki wa pop ilisema kuwa Mirziyoyev "hahitaji kutangazwa na msanii" baada ya mwimbaji mmoja kufyatua wimbo unaoitwa "Selfie with my President (Kujipiga Picha na Rais Wangu)". 

Wimbo huo ulikuwa ukichezwa mara kwa mara katika chaneli maarufu za burudani, lakini ulikuwa ukikosolewa na wengi kwenye mitandao ya kijamii.

Nchini Turkmenistan, nchi nyingine iliyokuwa ya kijamii barani Asia, mganga wa meno wa zamani, Gurbanguly Berdymukhamedov alikataza viongozi na vyombo vya habari kumsifu baada ya kuingia madarakani mwaka 2006.

Lakini taratibu alijikuta akikubaliana na hali hiyo akimfuata mtangulizi wake, Saparmurat Niyazov ambaye utawala wake wa mabavu ulikuwa ukilinganishwa na wa Korea Kaskazini.