Ramaphosa aapishwa Afrika Kusini

Saturday May 25 2019

 

Pretoria, Afrika Kusini. Rais Cyril Ramaphosa ameapishwa leo Mei 25 kuwa Rais wa Afrika Kusini kwa muhula wa pili.

Hafla ya kuapishwa kwake imeudhuriwa wa viongozi wa nchi mbalimbali, akiwamo Rais John Magufuli na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete na watu wanaokadiriwa kuwa 36,000 katika Uwanja wa Loftus Versfeld  jijini Pretoria.

Ramaphosa ameapishwa na Jaji Mkuu wa Afrika Kusini, Mogoeng Mogoeng.

Hafla hiyo ilipambwa na ndege za kijeshi zilizorushwa angani na askari waliotua kwa miavuli na mizinga ya heshima kwa Amiri Jeshi Mkuu.

Ramaphosa (66) mapema wiki hii alipitishwa moja kwa moja na Bunge la nchi hiyo baada ya chama chake cha ANC kushinda uchaguzi wa wabunge nchini Afrika Kusini kwa kupata viti 230 kati ya 400.

Ushindi huo ambao ni sawa na asilimia 57.5, ingawa unakiwezesha chama hicho kumteua rais kabla ya kuidhinishwa na Bunge, ni mdogo ambao chama hicho kimewahi kupata tangu mfumo wa ubaguzi wa rangi umalizike nchini humo miaka 25 iliyopita.

Advertisement