Ramsey amfuata Ronaldo Juventus

Thursday January 10 2019

 

London, England. Aaron Ramsey amekubali kutia saini mkataba wa miaka mitano kujiunga na Juventus ‘Kibibi Kizee’ ambapo atacheza pembeni na nyota Cristiano Ronaldo.

Ramsey anandoka Arsenal baada ya kuitumikia kwa miaka 10 akiwa analipwa mshahara wa Pauni140,000 kwa wiki.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales, alianza mazungumzo na klabu hiyo tangu msimu uliopita wa majira ya kiangazi baada ya kugoma kuongeza mkataba mpya Arsenal.

Ramsey na Arsenal walishindwa kuafikiana kuhusiana na suala la mshahara kabla ya Juventus na baadhi ya klabu za Ulaya kuanza kumnyemelea.

Mwandishi wa habari wa Italia, Fabrizio Romano, alisema kuwa pande hizo zimekubaliana Ramsey kuanza kuitumikia Juventus majira ya kiangazi.

“Aaron Ramsey atakuwa mchezaji wa Juventus Juni, mpango umekamilika. Wakala wake atakuwa Italia muda mfupi ujao kuzungumza na Mkurugenzi wa Juventus Fabio Paratici,” aliandika Romano katika mtandao.

 Mapema mwaka huu, Paratici alisema Ramsey ni mchezaji wa kiwango bora mwenye sifa ya kuwatumikia mabingwa hao wa Ligi Kuu Italia.

“Ni mchezaji hodari. Kwa miaka mingi amekuwa katika kiwango bora, mkataba wake ulipomalizika tulikuwa makini kumfuatilia,” alisema kigogo huyo.

Kiungo huyo mshambuliaji, amecheza mechi 252 na amefunga mabao 38 Arsenal tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea Cardiff City.


Advertisement