Rayvanny: Nilijua kwenye muziki ndio basi tena

Staa anayewakilisha lebo ya WCB, Raymond Mwakyusa maarufu Rayvanny amesema baada ya kufungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kujishughulisha na muziki alijua utakuwa mwisho wake kimuziki.

Desemba mwaka jana Rayvanny pamoja na Diamond wote kutoka lebo hiyo, walifungiwa kwa muda usiojulikana kufanya shughuli za sanaa baada ya kufanya makosa mbalimbali wakati wa tamasha la Wasafi ikiwamo kuimba wimbo wa Mwanza uliokuwa umefungiwa.

Hata hivyo, walifunguliwa Januari 23, mwaka huu, baada ya kuomba radhi kwa baraza hilo kwa kuandika barua kwa nyakati tofauti huku wakiahidi kubadilika.

Katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi, Rayvanny mkali wa vibao mbalimbali vikiwamo Zezeta, Chombo, Pochi Nene na Unaibiwa, alisema baada ya kufungiwa alipata wakati mgumu na kuona ndoto zake kwenye muziki ndio basi tena.

Mbali na muziki, pia anasema alijua asingeweza kuingia mikataba ya kufanya shughuli mbalimbali, kwani hata wadau huangalia uhai wa msanii kwenye tasnia hiyo.

Hata hivyo, anasema baada ya kufunguliwa anashukuru ngoma yake ya ‘Tetema’ aliyoifanya na Diamond imeweza kupokelewa vizuri na kumrudishia matumaini yaliyokuwa yameanza kupotea.

“Kwa kweli Tetema imenifanyia maajabu ambayo sikutegemea, kwani kwa siku nne tu tangu itoke imeweza kuangaliwa na watazamaji zaidi ya milioni moja huu kwangu ni ushindi mkubwa na imenipa moyo kwamba bado mashabiki wananihitaji,” alisema Rayvanny.

Msanii huyo alieleza kuwa aliyoyapitia yamemfundisha na kuapa kutorudia tena kwani ameona madhara ya kuwa nje ya muziki, kazi ambayo anaipenda na ameisotea hadi kufika hapo alipo.