Repoa yaishauri Serikali kuhusu soko la korosho

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua tafiti hizo, Naibu Waziri wa Kilimo, Bashungwa alisema licha ya kuonyesha kushuka kwa mauzo ya mazao nje ya nchi kumekuwapo na ongezeko la ukuaji wa sekta ya uchumi katika mauzo ya nje.

Dar es Salaam. Iwapo Serikali itawaachia uhuru wakulima wa korosho hususani katika biashara itaepusha mkanganyiko wa kibiashara na kutodumaza zao hilo.

Akiwasilisha utafiti wake jana, Dk Blandina Kilama alisema tofauti na Serikali ya Vietnam ambayo hujihusisha na sekta ya korosho kwa kutoa mbegu kutengeneza miundombinu, huduma za umeme, utafuti na uchakataji, Serikali ya Tanzania inasimamia moja kwa moja jambo linaloathiri.

“Ukiangalia mfano wa Tanzania ni rahisi kuona kwamba Serikali ikisimamia moja kwa moja inaweza kuwaza kukua kwa sekta ya korosho,” alisema.

Utafiti huo ni miongoni mwa tafiti zilizomo kwenye vitabu vinne vilivyozinduliwa jana na Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa jijini Dar es Salaam, uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umaskini (Repoa).

Mapendekezo ya utafiti huo ni Serikali kutoingilia sekta ya zao la korosho.

Utafiti huo uliolinganisha uzalioshaji wa korosho kati ya Tanzania na Vietnam umekuja wakati kukiwa na msukosuko wa soko baada ya Serikali kuingilia ununuzi wa zao hilo kutokana na wafanyabiashara kutangaza bei zilizokataliwa na wakulima.

“Utafiti huu wa korosho unaonyesha kwamba uhuru wa wakulima Vietnam kuchagua unawapa wachakataji changamoto washindane, ilhali uhodhi wa chombo kimoja cha Serikali kama ilivyo Tanzania ni kikwazo kikubwa kwa ukuaji wa sekta nzima,” alisema.

Mbali na zao la korosho, mkurugenzi wa Repoa, Dk Donald Mmari alisema kumekuwapo na anguko la mauzo ya mazao nje ya nchi, licha ya kuwepo kwa mageuzi ya mfumo yaliyoambatana na mabadiliko ya muundo wa bodi za mazao ambazo zilipewa mamlaka ya kudhibiti bei.

Aliyataja mazao yaliyoshuka kimauzo nje ya nchi kuwa ni korosho, pamba, kahawa, mkonge, chai na tumbaku aliyosema yameshuka kutoka asilimia 65 mwaka 1961 hadi asilimia 10 mwaka 2015. “Kushuka kwa viwango vya uzalishaji na ubora wa mazao kama kahawa kulichangiwa na hali ya kudhoofika kwa taasisi za kati hususan vyama vya ushirika na vyama vya msingi,” alisema.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua tafiti hizo, Naibu Waziri wa Kilimo, Bashungwa alisema licha ya kuonyesha kushuka kwa mauzo ya mazao nje ya nchi kumekuwapo na ongezeko la ukuaji wa sekta ya uchumi katika mauzo ya nje.

Mbali na Dk Mmari na Dk Kilama, watafiti wengine waliozindua tafiti zao ni pamoja na Dk Paschal Mihyo, Dk Lucas Katera na Dk Jamal Msami.