Rihanna awa milionea wa kike katika muziki duniani

Muktasari:

Anakadiriwa kuwa na utajiri wa Sh1.2 trilioni


Jarida la Forbes limemtangaza mwanamuziki Rihanna kuwa mwanamuziki wa kike milionea duniani akiwabwaga mastaa wenzake kama Madonna, Celine Dion na Beyonce.

Taarifa ya Jarida hilo iliyotoka jana imesema Rihanna ameshika nafasi ya kwanza akiwa na utajiri wa dola za Marekani milioni 600 ambao ni wastani wa Sh1.3 trilioni.

Mwanamuziki Madonna anamfuatia akiwa na utajiri wa dola za Marekani 570, Celine Dion akiwa na 450 na Beyonce akiwa na dola milioni 400.

Utajiri wa Rihanna unatajwa kutokana na biashara ya vipodozi vya Fenty Beauty  ambayo anaiendesha kwa kushirikiana na kampuni LVMH inayomilikiwa na bilionea wa Ufaransa, Bernard Arnault.

Staa huyo wa nyimbo Umbrella, Wild Thoughts, Rude Boy, Take a Bow na nyingine nyingi alianzisha kampuni ya vipodozi ya Fenty mwaka 2017 ambayo  ilimuingizia dola za Marekani 100 katika wiki ya kwanza ya mauzo.

Mpaka mwishoni mwa mwaka jana inakadiriwa kuwa kampuni hiyo anayoimiliki kwa asilimia 15 imemuingiza  iliingiza dola za Marekani 570 milioni.

Forbes pia inataja utajiri mwingine wa staa huyo kutoka visiwa vya Barbados kuwa unatokana na mauzo ya nguo za ndani za Savage X Fenty anazozitengeneza kwa ushirikiano na kampuni ya TechStyle Fashion Group.