MWANANCHI JUKWAA LA FIKRA: Rukwa na Katavi sasa wageukia kilimo cha kisasa kutoka kilimo cha mazoea

Rukwa na Katavi ni miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula kwa wingi. Hata hivyo, kabla mikoa hiyo haijagawanywa, ulikuwa ni mkoa mmoja wa Rukwa ambao ulikuwa miongoni mwa mikoa mitano inayozalisha chakula kwa wingi.

Mikoa mingine ni pamoja na Morogoro, Kigoma, Iringa, Ruvuma na Mbeya.

Licha ya uzalishaji mkubwa wa chakula, imebainika kuwa kilimo chake kilikuwa ni cha mazoea ambapo wakulima wengi walikuwa wakihama kutafuta maeneo yenye rutuba na hivyo wakawa wakiharibu mazingira.

Kilimo hicho si tu kwamba kilikuwa kikiharibu mazingira, bali pia kilikuwa kinatishia upungufu wa chakula kwa sababu ya kupoteza rutuba huku pia kukiwa na ongezeko la watu hasa wafugaji waliohama kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kutafuta malisho.

Kwa kuliona tatizo hilo, Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) linatekeleza mradi wa Sumbawanga na Katavi (Suka) wenye lengo la kuwaunganisha wakulima na kuwapa mafunzo ya kilimo cha biashara.

Mradi huo ulianzishwa Septemba 2017, lengo likiwa ni kuwafikia wakulima 122,000 na mazao yaliyopewa kipaumbele ni mpunga, mahindi na maharage.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana meneja wa mradi huo, Alinanuswe Mwalwenge anasema wamechagua mazao hayo kwa sababu si tu kwamba ni ya chakula bali pia ni mazao ya biashara.

“Kwa hiyo tukaona licha ya kuongeza usalama wa chakula tutainua kipato cha mkulima,” anasema.

Akizungumzia mafanikio ya mradi huo, anasema mpaka Machi 2019 wameweza kuwafikia wakulima 84,000 na kwa sababu ni mradi wa miaka mitatu wana uhakika wa kuwafikia wakulima waliopangwa yaani 122,000.

Akizungumzia maeneo wanayofanyia kazi, Mwalwenge anasema wanatoa huduma za ugani kwa kuwafundisha wakulima mbinu bora za kilimo na kuweka mashamba ya mfano (shamba darasa) ili waone.

“Tunahakikisha wanapata mbegu, mbolea na dawa zinazotumika shambani. Vilevile tunawafanyia mafunzo kama ushirika, elimu ya biashara.”

Katika eneo la masoko, Mwalwenge anasema mradi huo umekaa kimasoko ambapo kabla ya kulima wakulima huunganishwa na wanunuzi wa mazao na hivyo kuwa na uhakika kwa masoko.

“Kwa hiyo wakulima wanapata mafunzo ya pamoja, wanazalisha kwa pamoja mpaka kwenye soko. Tunachofanya ni kuwaunganisha wakulima katika vikundi, tunawafundisha, tunawaunganisha na wauzaji wa pembejeo na wanunuzi wa mazao.

“Hata kama kuna mahitaji ya mikopo, inakuwa rahisi kupata kwa sababu vikundi vimesajiliwa na vinatambulika,” anasema.

Mbali na masoko mradi huo umesaidia kukarabati maghala 25 kati ya 40 yaliyokuwepo na pia tumejenga maghala mapya katika mikoa hiyo, kwa mkoa wa Rukwa maghala matatu na Katavi maghala mawili.

“Sisi tunawafundisha wasihame kwa sababu hawatapata mavuno waliyokuwa wanapata. Mpaka sasa Rukwa na Katavi zimeongeza uzalishaji wa mahindi na mpunga,” anasema.

Anaongeza, “Mimi natoka Mbarali, lakini naweza kusema mpunga sasa unazalishwa zaidi Katavi. Wakulima walikuwa wakipata magunia kati ya saba hadi 14, lakini sasa wanavuna hadi magunia 25.”

Hata hivyo, anasema kumekuwa na uhamasishaji mkubwa wa uzalishaji wa mazao ya biashara na hivyo kuwafanya wakulima waachane na mazao ya chakula

“Kwa upande wa Katavi, wakati sisi tunahamasisha kilimo cha mahindi, mpunga na maharage, kumekuwepo na uhamasishaji wa mazao ya pamba na korosho. Sijui kama korosho itafanya vizuri, lakini pamba imekuwa ikifanya vizuri,’ anasema.

Wakizungumzia mradi huo, baadhi ya wakulima akiwemo Eutropia Sangu kutoka kijiji cha Isinde mkoani Rukwa anasema kwamba kabla ya mradi huo walikuwa wakilima maharage kienyeji na kwa kuhama hama.

“Baada ya mradi huu tumefundishwa mbinu mpya za kilimo ikiwa ni pamoja na matumizi ya mbegu bora na mbolea kiasi kwamba kumekuwa na mavuno mengi zaidi,” anasema Sangu.

Naye Samson Fyura kutoka kijiji cha Mtapenda Rukwa anasema kwamba kabla ya mradi huo walikuwa wanalima matuta na kupanda mazao ambapo waliishia kupata magunia matatu hadi matano ya mahindi kwa hekta moja.

“Kwa mbinu tulizopewa, kwa hekta moja tunazalisha kati ya magunia 20 hadi 25 ya mahindi. Mradi huu ni mzuri na tunaomba wengine pia wafundishwe zaidi ili wawe na mavuno ya uhakika,” anasema Fyura.

Stephania Chiza ofisa ugani wa kijiji cha Mtapenda Rukwa anasema hatua walizochukua ni pamoja na kutoa elimu ya kupima mashamba, matumizi ya viuatilifu na jinsi ya kupanda mazao na kutunza mazao kwa kuweka mbolea na ndipo unaona asilimia 90 ya mahindi yanastawi.

Naye ofisa ugani Edward Mwakagile kutoka mkoani Katavi anasema kwamba kabla ya kuanza kwa mradi walifanya utafiti kwa wakulina na kubaini kuwa walikuwa wakipata wastani wa magunia saba ya mahindi kwa hekta moja, lakini sasa wakulima hao hao wanavuna kati ya magunia 20 hadi 25 kwa hekta.