VIDEO: Rungwe ahojiwa polisi, aachiwa kwa kufanya mkutano wa ndani

Muktasari:

  • Polisi mkoa wa Kinondoni imemhoji na kisha kumwachia, Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma) Hashim Rungwe akituhumiwa kufanya mkutano wa ndani bila kibali.

Dar es salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma) Hashim Rungwe amehojiwa na Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni kwa kufanya mkutano wa ndani bila kibali.

Akizungumza baada ya kumaliza mahojiano hayo leo Jumatatu Juni 3, 2019 Rungwe amesema baada ya kuhojiwa kwa dakika 45 kwa kufanya mkutano wa ndani bila kibali ametakiwa kuandika maelezo ya yale aliyoyazungumza katika mkutano ule.

"Polisi wametaka kujua kwa nini tulifanya mkutano bila kibali, sisi tulikuwa tunawaeleza wananchi kuwa tunataka tume huru ya uchaguzi," amesema Rungwe

"Kila uchaguzi namba ya wapiga kura inazidi  ikipungua ukituambia sisi tuwaache wananchi tayari tume imesema watu walewale watasimamia uchaguzi," ameongeza

Rungwe amesema baada ya kuhojiwa ameachiwa na hajaambiwa arudi tena kuripoti.

Mwenyekiti huyo amesindikizwa na viongozi kadhaa wa chama chake  pamoja na Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa.

Katika mkutano uliomfanya akahojiwa, ulifanyika jana Jumapili Juni 2, 2019 katika makao makuu ya Chaumma viongozi wa vyama nane vya upinzani walitoa tamko la kutoshiriki kwenye uchaguzi wa marudio kwenye kata 32 unaotarajiwa kufanyika  Juni 15, 2019 kwa sababu unasimamiwa na Wakurugenzi Halmashauri za wilaya na Manispaa kinyume na uamuzi wa Mahakama Kuu

Wawakilishi wa vyama hivyo ni vyama vya ACT Wazalendo, CCK, Chadema, DP, NCCR Mageuzi, NLD na UPDP.