Ruto apuuza vita vya ufisadi Kenya

Muktasari:

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto amepuuzia mbali kampeni inayoendelea nchini humo dhidi ya ufisadi akisema ni propaganda zinazoendeshwa na “vibaraka waliopoteza mwelekeo.”

Nairobi, Kenya. Naibu Rais wa Kenya, William Ruto amepuuzia mbali kampeni inayoendelea nchini humo dhidi ya ufisadi akisema ni propaganda zinazoendeshwa na “vibaraka waliopoteza mwelekeo.”

Ruto alisema watu hao wanaongozwa na chuki, uongo, nia mbaya ya kuwapumbaza wananchi wasione mazuri yanayofanywa na serikali ya Jubilee.

Vita dhidi ya ufisadi nchini Kenya iliasisiwa na Rais Uhuru Kenyatta na ameapa kwamba hatalegeza kamba.

Akizungumza katika Uwanja wa Rurinja, mjini Njabini, Kaunti ya Nyandarua ambako aliapa kuendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo ya Kanisa Jumamosi Julai 27, Ruto alisema wale wanaopaza sauti kuhusu ufisadi serikalini, wanafaa kujadili utendakazi wa serikali na mafanikio yake.

“Wanazunguka kote nchini wakieneza propaganda kuhusu ufisadi, nawaambieni ya kwamba ni watu waovu wenye kijicho. Wanataka ionekane kana kwamba serikali haifanyi kazi na kwamba ufisadi umekithiri. Wapuuzeni kwani ni vibaraka waliopoteza mwelekeo,” alisema Ruto.

Alisema miradi yote ya serikali inaendelea ilivyopangwa na hakuna iliyokwama kwa ukosefu wa fedha.

Kauli ya Ruto imekuja siku tatu baada ya Waziri wa Fedha, Henry Rotich na maofisa wakuu wa wizara hiyo kusimamishwa kazi baada ya kushtakiwa kuhusiana na sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwerer. Inadaiwa Sh21 bilioni zilipotea.

“Wajibu wangu kama Naibu Rais ni kusimamia miradi hiyo na kuhakikisha imetekelezwa ilivyopangwa bila hitilafu. Tumejitolea kutimiza ahadi zetu. Wale wanaohubiri kuhusu ufisadi sharti waelewe haya. Watu wa Nyandarua na Wakenya ni mashahidi wa utendakazi mzuri wa serikali,” akasema.

Ruto alisema madai kuhusu ufisadi yameshamiri utadhani serikali haifanyi kazi, akiongeza kuwa, mjadala kuhusu ufisadi unalenga kuhujumu ajenda ya maendeleo ya serikali.

“Nawahakikishia kuwa Kenya iko katika mkondo mzuri, tumetekeleza miradi ya maendeleo katika pembe zote nchini,” alieleza.

Vilevile, Ruto ametoa kauli hiyo siku moja baada ya watu wake wa karibu kutoka ngome yake ya Rift Valley kukejeli vita dhidi ya ufisadi wakisema vinaendeshwa kwa njia isiyozingatia usawa.

Wakizungumza katika Jimbo la Kesses, kaunti ya Uasin Gishu, wabunge Oscar Sudi  wa Jimbo la Kapseret), Nelson Koech (Belgut), Hillay Kosgei (Kipkelion Magharibi) na Catharine Waruguru (Laikipia) walidai “watu fulani wanaachwa” katika vita dhidi ya uporaji mali ya umma.

“Mtindo unaotumiwa hapa ni ule wa shamba la wanyama. Kuna wanyama wengine ambao ni bora kuliko wenzao… hakuna haki kwani wahusika wengine wa ufisadi bado wako huru huku Rotich na Thugge wakifikishwa kortini,” alisema Kosgei.