SADC: Tanzania imejitahidi usawa wa kijinsia

Muktasari:

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika kuthamini nafasi ya mwanamke katika nafasi za uongozi tangu mwaka 2005 hadi 2019.


Kutokana na hatua hiyo, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika usawa wa kijinsia

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema Tanzania imepiga hatua katika kuthamini nafasi ya mwanamke katika jamii na ngazi za uongozi  ikilinganishwa na miaka 14 iliyopita.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 14, 2019 wakati wa uzinduzi wa machapisho matano yanayoelezea mikakati inayojikita zaidi katika kutazama nafasi ya mwanamke katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Ripoti hizo tano zinatoa uelekeo wa  nafasi ya mwanamke katika masuala ya ulinzi na usalama, maendeleo ya kiuchumi, nafasi za uongozi, ufuatiliaji wa sekta ya nishati na miundombinu.

Kupitia machapisho hayo, Waziri Ummy ameeleza hali halisi ya Tanzania katika nyanja hizo akielezea ukuaji wa thamani ya mwanamke kutoka mwaka 2005 mpaka 2019 katika nafasi zote nyeti.

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika nafasi za uongozi, kwa mara ya kwanza mwaka 2015 tumempata Makamu wa Rais mwanamke, Mama Samia Suluhu Hassan, lakini ukiangalia katika Bunge la Tanzania mwaka 2005 kulikuwa na asilimia 22 pekee ya wanawake lakini kwa sasa ni asilimia 37,” amesema na kuongeza;

“Idadi ya mawaziri wanawake imeongezeka kutoka nikiwemo mimi, lakini pia majaji mwaka 2005 walikuwa asilimia 34 lakini mwaka 2019 ni asilimia 34.”

 

Aidha, Waziri Ummy amesema uwepo wa elimu bure katika shule za msingi na sekondari, imesaidia watoto wa kike wengi kwenda shule kwani mwaka 2019 watoto 8.2 milioni waliandikishwa kujiunga darasa la kwanza huku sekondari wakifikia 1.9 milioni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hizo, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Dk Stergomena Tax amesema katika nchi ambazo zimefanikiwa kuweka usawa wa kijinsia ni pamoja na Afrika Kusini na Sychelles, huku Tanzania ikiwa katika nafasi nzuri kufikia viwango.

Ripoti hizo tano ni pamoja na Mkakati wa wanawake katika ushiriki wa masuala ya ulinzi na usalama ndani ya SADC, Mkakati wa ufuatiliaji wa Maendeleo ya Jinsia wa SADC, Mpango wa Kushughulikia ukatili wa kijinsia katika SADC, Mpango wa ufuatiliaji sekta ya Nishati na Tathmini ya Mpango mfupi ya uendelezaji miundombinu.

Uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere(JNICC), Dar es Salaam nchini Tanzania umetanguliwa ikiwa ni siku tatu kabla ya ratiba ya Mkutano Mkuu wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 16 za Jumuiya hiyo.