Sababu Halima Mdee kuitwa polisi hii hapa

Muktasari:

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee leo Jumamosi Februari 23, 2019 hadi saa 8:00 mchana alikuwa akiendelea kuhojiwa na mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kinondoni (RCO) kwa kosa la uchochezi

Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee leo Jumamosi Februari 23, 2019 hadi saa 8:00 mchana alikuwa akiendelea kuhojiwa na mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kinondoni (RCO) kwa kosa la uchochezi.

Akizungumza na Mwananchi leo wakili Hekima Mwasipu amesema Mdee ameitwa polisi kwa kosa la uchochezi.

Hekima amesema kwa sasa polisi wanaendelea kumhoji kutokana na kauli alizozitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mikocheni Februari 21, 2018.

"Polisi wamemuita kwa kosa la uchochezi kutokana na kauli alizozitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mikocheni juzi tunaendelea kuandika maelezo,” amesema.

Mdee aliyefika kituo cha Polisi Oysterbay zilipo ofisi za RCO saa 3 asubuhi, alianza kuhojiwa  saa 6:15 mchana.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) alieleza kuitwa kwake kituoni hapo kupitia akaunti yake ya Twitter, “Nimepokea wito kituo cha Polisi Oysterbay kwa mahojiano.”