Sababu kuongezeka uzalishaji wa mazao Tanzania yatajwa

Saturday July 20 2019

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Japhet Hasunga amesema usimamizi na utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali vimechangia kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa mazao nchini Tanzania.

Amebainisha kuwa tathmini iliyofanywa na Wizara hiyo Mei hadi Juni 2019 kuhusu hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2018 hadi 2019 inaonyesha uzalishaji utafika tani 16.4milioni, mazao ya nafaka yakiwa zaidi ya tani 9milioni na yasiyo ya nafaka tani7.4 milioni.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Julai 20, 2019 katika  mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akitoa taarifa kuhusu hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2018 hadi 2019.

Amesema  uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuwa nzuri katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kufuatia uzalishaji wa ziada wa mazao ya chakula kuanzia msimu wa kilimo wa 2013 hadi 2014 na 2017 hadi 2018.

Amesema katika kipindi hicho nchi inajitosheleza kati ya asilimia 120 hadi 125 na inazalisha ziada ya kati ya tani 2,582,717  hadi  3,322,689.

“Katika tathmini ya hali ya chakula hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na usalama wa chakula tunaangalia baadhi ya mazao muhimu yanayohitajika zaidi kama mahindi, mtama, mchele, ngano, ndizi na muhogo,” amesema Hasunga.

Advertisement

Katika hatua nyingine, Hasunga amewataka wakulima nchini kuzalisha mazao ya chakula kwa kuzingatia kanda za kielojia pamoja na kuwa na hulka ya kuhifadhi chakula kulingana na mahitaji.

Lengo la kufanya hivyo ni kutumia mazao ya chakula kilichopatikana kiweze kutumika msimu mwingine wa uzalishaji.

 


Advertisement