Sababu nne uchumi wa Tanzania kukua hizi hapa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka wa fedha 2018 na mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri Wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ametaja sababu nne zilizochochea ukuaji wa pato halisi la Taifa kutoka asilimia 6.8 mwaka 2017 hadi asilimia 7.0 mwaka 2018, ikiwemo ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege.


Dodoma. Serikali ya Tanzania imetaja sababu nne za pato la Taifa kukua  kwa asilimia 7.0 mwaka 2018 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.8 mwaka 2017.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 13, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango  wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa  mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/2020.

Ametaja sababu hizo kuwa ni kuongezeka kwa uwekezaji hususan katika miundombinu kama ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege.

“Sababu nyingine ni kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme, kuimarika kwa huduma za usafirishaji na hali nzuri ya hewa iliyopelekea uzalishaji mzuri wa chakula na mazao mengine ya kilimo, “ amesema Dk Mpango.

Amesema shughuli za uchumi zilizokuwa kwa kasi na kiwango cha asilimia katika mabano ni; Sanaa na burudani (13.7), ujenzi (12.9), uchukuzi na uhifadhi mizigo (11.8); shughuli za kitaaluma, sayansi na ufundi (9.9); habari na mawasiliano (9.1), sekta ya kilimo (5.3) huku zilizotoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa zikiwa ni kilimo (asilimia 28.2), ujenzi (13.0) na biashara na matengenezo (9.1).