Sababu tatu zilizoibeba Simiyu kidato cha nne 2018

Tuesday February 19 2019

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Taja kila sababu ikiwamo ya uongozi bora, lakini ukweli ni kuwa Mkoa wa Simiyu unakuja kwa kasi kitaaluma.

Kutoka nafasi ya 14 kwa miaka miwili mfululizo (2015 na 2016) katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, Simiyu unaosifika kwa kuwa na uongozi wenye dira ya maendeleo, umepanda kwa nafasi nne na hivyo kuwa mkoa wa tisa mwaka 2018.

Ndiyo mara yake ya kwanza kuingia katika orodha ya mikoa kumi bora tangu kuwa na hadhi ya mkoa mwaka 2012.

Imeingia katika orodha hiyo ambayo imeshuhudia mikoa ya Pwani, Kigoma na Shinyanga ikiendelea kutamba kwa kuwamo katika orodha hiyo kwa miaka mingi. Mikoa mingine imekuwa ikiingia na kutoka.

Sababu za mafanikio

Mkuu wa mkoa huo, Antony Mtaka anataja sababu tatu kuwa ndizo nguzo za mafanikio hayo, ikiwamo ya uanzishwaji wa kambi maalumu kwa watahiniwa.

Anasema kambi hiyo ilikuwa kuwa na lengo la kuwaweka pamoja wanafunzi wanaofanya mtihani wa kitaifa ili kuwafundisha , kuwapa moyo na kuwajengea uwezo wa kujiamini utakaowasaidia kufaulu.

“Niliamua kufanya tathmini kwa nini Simiyu inafanya vibaya katika mitihani ngazi mbalimbali. Miongoni mwa mambo niliyoyagundua ni baadhi ya watoto kukosa muda sahihi wa kusoma kwa ufanisi kutokana na hali halisi ya mazingira ya vijijini ambapo wanachukuliwa na watu wa kufanya kazi baada ya kurudi shule,”anasema.

Mkuu wa mkoa huyo, anafafanua kuwa mazingira ya vijijini ni magumu hasa kwa watoto wa shule ambao baadhi yao wanaishi kwenye nyumba za tembe ambazo ndani yake wanalala na mifugo jambo linalosababisha kukosa muda wa kujisomea kwa ufanisi hasa nyakati za usiku.

“Hata hivyo, kwenye kambi hii maalumu wanafunzi wanapata muda mzuri wa kusoma na kubadilishana mawazo na wenzao wa mbalimbali .

‘‘Muda wao wa kusoma ni tofauti na wanafunzi wengine, wao wanaanza saa 1asubuhi hadi saa 12 jioni huku wengine wakianza saa 2 asubuhi hadi saa tisa alasiri, vivyo nyakati za usiku, ”anafafanua.

Mtaka anasema kambi hiyo inakuwa na walimu bora wanaowafundisha mada ngumu ambazo baadhi ya wanafunzi ya hawakuzielewa kwa ufanisi walipofundishwa katijka shule zao.

Mtaka anasema mkoa huo umeweka utaratibu wa baadhi ya watu maalumu wakiwamo wakuu wa wilaya na viongozi kwenda kuwatembelea kwa ajili ya kuwapa moyo wanafunzi hao na kuwaeleza mchakato wa elimu waliopitia hadi hapo walipo.

Ofisa Elimu wa mkoa wa Simiyu, Ernest Inju anasema kambi hizo, zimechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya elimu na kupandisha ufaulu wa mkoa huo kwa sababu zimeleta mwamko wa watoto kusoma kwa bidii

“Kwenye kambi kuna na walimu wa aina tofauti wanaofundisha wanafunzi hao masomo mbalimbali. Mfano kama wanafunzi wa shule fulani walikosa mwalimu wa hesabu au hawakufundishwa kwa ufanisi, wakiwa kambini wanapata ufahamu wa somo husika,”anasema.

“Kwenye kambi kuna na walimu wa aina tofauti wanaofundisha wanafunzi hao masomo mbalimbali. Mfano kama wanafunzi wa shule fulani walikosa mwalimu wa hesabu au hawakufundishwa kwa ufanisi, wakiwa kambini wanapata ufahamu wa somo husika,”anasema.

Ushirikiano wa wazazi na uongozi

Anaitaja sababu ya pili kuwa ni ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na uongozi wa mkoa katika suala la kuchangia shughuli za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Anasema wazazi wa mkoa wamekuwa mstari mbele kutoa ushirikiano katika sekta ya elimu ikiwemo kuhudhuria vikao vya kupanga mikakati ya kuboresha sekta hiyo kwenye mkoa huo.

“Nikiwa na watendaji wangu nilikutana nao na kuweka vipaumbele mbalimbali ikiwemo elimu na kilimo. Walionyesha ushirikiano katika suala hili, tuliamua kuwekeza katika kilimo nikiwa na maana ya kuwa watoto wakipata chakula cha kutosha ni rahisi kufanya vizuri masomo yao,’’ anasema.

Mtaka anasema kumekuwa na ushirikiano mkubwa kati yao na wazazi katika kuboreha sekta ya elimu mkoani humo na kwamba hivi sasa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa walezi, wazazi na wadau wanaoichangia kambi hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanaishi vizuri.

Sababu ya tatu anasema ni utayari wa wanafunzi wenyewe wa mkoa ambao wanaonyesha nia ya kusoma na kuleta mapindunzi na mabadiliko kuanzia ngazi za familia zao na mkoa kwa ujumla.


Advertisement