Sababu ujenzi Terminal III kusimama mwaka 2016 yatajwa

Ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale

Muktasari:

Ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale  ametaja sababu ya jenzi wa jengo la tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kusimama mwaka 2016

Dar es Salaam. Ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale  ametaja sababu ya jenzi wa jengo la tatu la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kusimama mwaka 2016.

Amesema sababu hiyo ni mkandarasi kudai kiasi cha fedha kilichokuwa kimebakia huku akiwa amefanya kazi kwa asilimia 55.

Mfugale ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Agosti Mosi, 2019 katika uzinduzi wa jengo hilo litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia watu milioni sita kwa mwaka wanaokwenda nje ya nchi. Abiria wanaofanya safari za ndani ya nchi watatumia jengo la pili la JNIA.

Amesema hadi  mwaka 2016, mkandarasi huyo ambaye ni Bam  International wa  Uholanzi  alikuwa amelipwa Sh380 bilioni na kudai Sh29 bilioni.

“Februari 8, 2017 baada ya Rais Magufuli (John) kufanya ziara ya kushtukiza katika jengo hili, alishangazwa na gharama hiyo na kuagiza kufanyika kwa mapitio ili kuona kama gharama ni halisi.”

“Uliagiza (Magufuli) mara moja kuwepo timu ya watalaam iliyogundua fedha hizo zimelipwa na hata mkandarasi angesimamishwa ingekuwa hasara kwa Serikali na ukaamua katoa fedha yote ambayo mkandarasi alikuwa anadai ndipo akarudi na leo tuko hapa,” amesema Mfugale.

Amesema hadi kukamilika kwa jengo hilo mkandarasi amelipwa Sh687.4 bilioni wakati mshauri mwelekezi akilipwa Sh13.1 Bilioni na ujenzi kwa ujumla ulikadiriwa kugharimu Sh705 bilioni.

Amesema kati ya fedha hizo,  Sh560 bilioni zinatokana na mkopo kutoka benki ya biashara ya Hongkong and Shanghai Bank Corporation (HSBC) ya China.