Safari za bila kuaga za mkurugenzi Siha zamshtua Majaliwa

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Siha, Valerian Juwal

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekerwa na safari za mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Siha, Valerian Juwal akibainisha kuwa amekuwa chanzo cha uzorotaji wa ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo.

Siha. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekerwa na safari za mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Siha, Valerian Juwal akibainisha kuwa amekuwa chanzo cha uzorotaji wa ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumapili Februari 24, 2019 wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo akiwa katika siku yake ya mwisho ya ziara yake mkoani Kilimanjaro.

Amebainisha kuwa lengo la kumleta mkurugenzi huyo Siha ni kuhakikisha anasimamia shughuli za maendeleo.

Awali, mkurugenzi huyo alipoulizwa na Majaliwa sababu za  mapato katika halmashauri hiyo kushuka hadi asilimia 38 mwaka 2017/18, alisema ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, kwamba wananchi wameshindwa kuvuna mazao ambayo wangeweza kukusanya ushuru.

"Acha visingizio sikiliza nikwambie mkurugenzi tatizo lako unasafiri sana husimamii shughuli za maendeleo katika halmashauri yako, huko unakoenda unaitwa na nani," amesema Majaliwa.

 

"Rais (John Magufuli)  amekuleta usimamie halmashauri hii lakini kila siku unasafiri. Niambie ni lini kwenye safari zako ulimuaga mkuu wa wilaya au katibu tawala wa mkoa?"

 

Majaliwa amesema anatilia shaka uhusiano wa mkurugenzi huyo na mkuu wa wilaya hiyo, Onesmo Buswelu.

 

"Msipokuwa serious (makini) hamuwezi kufikia malengo na mnapokosa seriousness tutawawajibisha, na hii nikisikia tena nitafanya maamuzi," amesema Majaliwa.