Samatta: Stars imepata kipimo sahihi kwa Misri - VIDEO

Muktasari:

Taifa Stars itacheza mechi nyingine ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Zimbabwe Jumapili usiku.


Nahodha wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta amesema kuwa wamepata kipimo sahihi katika mchezo wao dhidi ya magwiji wa soka wa bara la Afrika, Misri licha ya kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa jana usiku.

Katika mechi hiyo, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Borg El Arab, Misri ilifunga bao la ushindi  dakika ya 65 kupitia kwa beaki wa kushoto Ahmed Elmohamady.

Elmohamady, ambaye anachezea timu iliyopanda Ligi Kuu ya England  Aston Villa, alifunga kwa kichwa mbele ya kiungo wa Tanzania, Farid Mussa anayechezea timu ya DC Tenerife ya Hispania.

Samatta alisema kuwa wameona makosa yao na anaamini benchi la ufundi chini ya kocha, Emmanuel Amunike watayarekebisha kabla ya mchezo wao wa pili wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe utaochezwa Jumapili usiku kabla ya mashindano ya AFCON yaliyopangwa kuanza Juni 21.

Pamoja kupoteza mchezo huo, ambao nyota wa Misri, Mohammed Salah hakucheza, Taifa Stars ilicheza vizuri na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga na kushindwa kuzitimua.

“Hiki ni kipimo sahihi kwetu, mechi hii imeonyesha jinsi gani mashindano haya ni magumu, naamini kocha na wenzake watafanya marekebisho kabla ya mashindano,” alisema Samatta.

Alisema kuwa wachezaji wameonyesha ukakamavu mkubwa katika mchezo huo ambao Amunike alifanya mabadiliko mawili tu, kumtoa John Bocco na Farid Mussa na nafasi zao kuchukuliwa na Thomas Ulimwengu na Mohammed Hussein.