Samia Suluhu, Makamba wampongeza Kapuya kwa kuoa

Muktasari:

 

  • Si unajua kuwa mbunge wa zamani wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya mwenye umri wa miaka 73 alimuoa binti anayedaiwa kuwa na miaka 25. Basi leo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wamempongeza kwa uamuzi wake huo.

Tabora. Unaweza kusema Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wamempongeza mbunge wa zamani wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya kwa kuoa.

Pongezi hizo zimetolewa baada ya Profesa Kapuya kuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano wa Makamu wa Rais uliofanyika Kaliua mkoani Tabora leo Jumapili Februari 24, 2019.

Waziri huyo wa zamani wa elimu mwenye umri wa miaka 73 hivi karibuni alimuoa Mwajuma Mwiniko anayedaiwa kuwa na miaka 25 na kuzua gumzo.

Binti huyo ni mtoto wa Athuman Mwiniko ambaye ni diwani wa Mchikichini wilayani Urambo.

Akizungumza katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wananchi, Samia Suluhu amesema alifanya kazi na Profesa Kapuya miaka ya nyuma katika Wizara inayosimamia masuala ya Muungano.

Amesema kwa sasa Profesa Kapuya amepiga hatua zaidi na kuwafanya wananchi kuangua kicheko huku akiwataka wanawake waliokuwepo eneo hilo kumpigia makofi na kumshangilia mbunge huyo wa zamani, jambo ambalo walilifanya.

Awali, Makamba alimpongeza Kapuya kwa uamuzi wake wa kuoa akibainisha kuwa utamfanya aongeze miaka ya kuishi na kumtakia kila la kheri.

Februari 21, 2019 Kapuya alizungumza na Mwananchi na kubainisha kuwa anashangaa ndoa yake na Mwajuma kuzua gumzo wakati hajavunja sheria au kukiuka taratibu zozote za nchi.

“Kwani wanataka nioe mwanamke mwenye umri sawa na bibi yangu,” amehoji.

Kapuya amesema umri hauhusiani na mapenzi, hivyo watu wakubali matokeo kwani hajamtorosha shule mwanamke huyo, wala hajavunja sheria, mila, desturi au misingi  ya dini.

“Nimevunja sheria, nimekiuka maadili, nimemuachisha shule  Hapana,” amesema  Kapuya ambaye pia amewahi kumiliki bendi maarufu ya muziki wa dansi ya Akudo.

Waziri huyo wa zamani amesema Mwajuma ni mkewe wa pili na kubainisha kuwa hataongeza mwingine.

“Siwezi tena kuoa mwanamke mwingine kwani mke huyu ni somo tosha, sababu mke wangu wa kwanza anaishi Dar es Salaam na nampenda sana. Hapa subirini tu mtoto kutoka kwa huyu mwanamke mnayesema ana umri mdogo," amesema Kapuya.

Akizungumzia alivyokutana na mkewe, Kapuya amesema alimfahamu alipokuwa anakwenda kufanya vikao akitokea Urambo.