Samia asema Tanzania imefanikiwa mapambano ya dawa za kulevya

Wednesday June 26 2019

By Burhani Yakub, Mwananchi [email protected]

Tanga. Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imeingia katika rekodi ya nchi iliyofanikiwa vita ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya baada ya kuwakamata vigogo wa biashara hiyo ambao miaka ya nyuma walishindikana.

Samia amesema hayo leo Jumatano Juni 26, 2019 wakati wa maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya Duniani uliofanyika kitaifa Jijini Tanga.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema kukamatwa kwa matajiri ambao wanatajwa kuhusika na usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya ni hatua kubwa ambayo kutokana na fedha walizonazo ilikuwa vigumu kuwakamata.

"Vita ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya haiwezi kufanikiwa kama rushwa katika nchi haitadhibitiwa kwa sababu vigogo wa biashara ya dawa za kulevya wako tayari kuhonga kiasi chochote cha fedha ili kuhakikisha inaendelea,” amesema Mkuchika

Amesema jamii inapaswa kushiriki kikamilifu katika vita ya kupiga dawa za kulevya kwa kuwa yanawaharibu vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.

Mkuchika amesema Serikali ya awamu ya tano itahakikisha inawakamata vigogo wote wa biashara hiyo ili kuiwezesha Tanzania kuwa nchi isiyo dawa hizo haramu.

Advertisement

Naye Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Valise Kashusa ametaja baadhi ya changamoto zinazodhoofisha mapambano ya dawa za kulevya  ni uzalishaji wa dawa mpya (Synthetic drugs) zinazotengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu, kuongezeka kwa matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya mfano penthedine, ketemine, tramodol na Valium kama mbadala wa dawa za kulevya.

Pia amesema kuongezeka kwa uzalishaji wa dawa za kulevya duniani hivyo kuiweka nchi katika mazingira hatarishi ya kuendelea kusakamwa na uingizaji wa dawa hizo.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema wizara yake imekuwa ikijitahidi kuhakikisha nyumba za kuwalea waathirika wa dawa za kulevya walioamua kuacha zinapata dawa za kutosha.

Advertisement