Samia ataka idadi ya wanawake waliopo kwenye uongozi ibainishwe

Wednesday August 14 2019

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelitaka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake Duniani  (UN WOMAN)  kuandaa tathmini ya nchi kuhusiana na Kongamano la Beijing.

Amesema ni vyema kuwepo na uwezekano wa kuandaa tathmini ya uhakika itakayoweza kuonyesha hali halisi ya idadi ya wanawake waliopo katika nafasi mbalimbali za uongozi hususani kwenye mashirika na taasisi binafsi.

Samia ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 14, 2019 alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa UN WOMAN Hodan Addou ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolea na ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania inaeleza  kiongozi huyo amelishukuru UN WOMAN kwa kuendelea kutoa fursa katika nyanja mbalimbali za kijamii na kimaendeleo kwa wanawake duniani na kulitaka kuendelea kuzidi kutoa fursa hizo hususani kwenye sekta za Kilimo.

Naye Addou aliyeambatana na Mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB) Denis Biseko  amemshukuru Samia kwa kuimarisha ulizi wa masoko kwa kuzuia utumikishaji wa wanawake na watoto katika masoko.

Shirika hilo kwa kushirikiana na WB limeandaa warsha itakayozungumzia mambo mbalimbali ikiwemo wanawake kutambua hali zao katika biashara.

Advertisement

Advertisement