Samia kufungia kongamano la nchi sita Kigoma

Monday April 15 2019

 

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika kongamano la wafanyabiashara la nchi zinazozunguka ziwa Tanganyika linalotarajia kufanyika siku tatu kuanzia Mei 9 hadi 11, 2019 mkoani Kigoma.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili 15, 2019, Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Emanuel Maganga amesema nchi zitakazoshiriki kongamano hilo ni pamoja na Zambia, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Tanzania.

Mkuu wa mkoa amesema kongamano hilo la kwanza kufanyika mkoani humo lina lengo la kuwakutanisha Wafanyabiashara na kujadili fursa zilizopo nje na ndani ya nchi ili kunufaika.

"Kongamano hili linatarajiwa kuudhuriwa na  watu zaidi ya 300 ambapo malengo makuu ni pamoja na kuanzisha mahusiano na nchi za maziwa makuu pamoja na kuimarisha biashara za mipakani," amesema Maganga.

Naye ofisa biashara mkoa, Deogratius Sangu amewataka wafanyabiashara wadogo wa mkoa huo kutumia fursa hiyo kujitangaza bila kusahau vitambulisho walivyopatiwa na Rais John Magufuli ili kuweza kutambulika.

Mwenyekiti wa Jukwaa la wafanyabiashara (TCCIA) mkoa wa Kigoma, Ramadhani Gange, amesema Kongamano hilo litasaidia kuondoa usumbufu wanaoupata wakati wa kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi ikiwemo ukubwa wa kodi na tozo.

Advertisement