Sarakasi za korosho zilivyovuma bungeni, kutikisa mawaziri

Saturday November 24 2018

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Msimu wa mauzo ya korosho kwa mwaka 2017/18 umekuwa na misukosuko mingi kiasi cha kuifanya Serikali kuingilia kati ikitumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kununua na kudhibiti biashara ya zao hilo.

Mivutano ilianza kuonekana mapema ambapo Mei mwaka huu katika Bunge la Bajeti, Mbunge wa Mtama, (CCM), Nape Nnauye alishikilia shilingi ya mshahara wa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba (sasa ameondolewa) kwa kutoridhishwa na majibu ya Serikali kuhusu fedha za ushuru wa mauzo ya nje ya korosho (export levy).

Wiki moja baadaye Mei 24, Nape aliibua tena hoja hiyo na kumfanya Spika Job Ndugai kutoboa siri ya Waziri Tizeba kulia kama mtoto mbele ya Kamati ya Bajeti ya bunge hilo.

Katika hoja yake, Nape alisema kulikuwa na ugonjwa unaoshambulia korosho lakini bei ya dawa yake aina ya salfa iliyotakiwa kuuzwa Sh16,000 kwa mfuko, imefika Sh75,000.

Kwa sababu hiyo, Nape alisema hakuna namna mkulima anaweza kugharamia, hivyo alimwomba Spika Bunge kujadili suala hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Jenista Mhagama alifafanua kuwa Serikali ilikuwa imeagiza kutoa Sh10 bilioni kwa ajili ya kazi hiyo na fedha hizo zimeshatolewa.

Mabadiliko ya sheria

Suala hilo halikuishia hapo, Serikali ilikwenda Iliamua kuibadilisha Sheria ya Tasnia ya Korosho Na. 18 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 kwa kuongeza kifungu Na. 17A ambacho kilitoa mamlaka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kukusanya ushuru wote wa korosho ghafi zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi na kuingizwa katika mfuko wa Serikali.

Kifungu hicho awali kilikuwa kinaelekeza fedha za ushuru huo asilimia 65 ziingie kwenye Mfuko wa Kuendeleza zao la korosho kwa ajili ya kuendeleza zao na asilimia 35 ziingie katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mabadiliko ya sheria hiyo yalizua mvutano mkali bungeni Dodoma Juni 25, 2018.

Nape alibainisha kuwa ukizungumzia korosho unazungumzia maisha ya watu katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na mingine inayolima korosho.

Katika mjadala huo, Ghasia aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kabla ya kujiuzulu baadaye alisema kuna wabunge wamekaa vikao wameandaliwa kuwadhalilisha wabunge wenzao wanaowatetea wakulima.

“Niwahakikishie wakulima wanaolima korosho, wabunge wao tutapambana, hata haki isipopatikana ila tutawatetea,” alisema Ghasia.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge waliiunga mkono Serikali kuhusu ushuru huo akiwamo Mbunge wa Morogoro Kusini, Omary Mgumba aliyesema hoja ya kutetea mikoa miwili inaweza kuligawa Taifa.

“Nimekaa kwenye korosho miaka 19, sheria ilianza mwaka 1984 baada ya zao hili kudorora nchini, tulifika uzalishaji wa tani 174,000, tukashuka mpaka tani 16,000 kwa mwaka, ndipo Serikali ya awamu ya kwanza ikaamua kuja na mkakati maalumu wa kufufua zao hili,” alisema Mgumba.

Wakati malumbano hayo yakiendelea bungeni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya vikao na wabunge wa mikoa ya kusini inayozalisha korosho akiwasihi kulegeza msimamo wao, lakini walikataa katakata.

Wabunge hao waliendelea na kampeni yao hata nje ya Bunge ikiwa pamoja na kufanya mikutano na vikundi vya wakulima mjini Dodoma.

“Wakipitisha sheria hii tayari tumeshakatwa miguu kwani hatutaweza tena kudai hizo fedha,” alisema Daimu Mpakate, mbunge wa Tunduru Kusini (CCM).

Wakizungumza jijini Dodoma viongozi wa vikundi vya wakulima wa korosho nchini walisema Serikali isipowasikiliza italiangamiza zao hilo.

Mwenyekiti wa Chama cha wakulima wa Tandahimba (Tafa), Faraji Njapuka alisema wamekuwa wakikatwa Sh10 kwa kila kilo ya korosho kwa ajili ya maendeleo ya korosho wakati uliokuwa Mfuko wa wakfu wa kuendeleza zao la korosho (CIDTF) ulishafutwa.

Mwenyekiti wa Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (Mviwata), Abdul Gea alisema wakulima wana haki ya kudai asilimia 65 ya mgawo wa ushuru kwa sababu ni ya kwao na Serikali isipotoa fedha hizo italiangamiza kabisa zao la korosho. Licha ya malumbano hayo, Bunge lilipitisha marekebisho ya sheria hiyo na kuifanya Serikali kuchukua fedha hizo kwa asilimia 100.

JPM awaonya wabunge

Baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo, Rais John Magufuli alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, Julai 1, 2018 ambayo pamoja na mawaziri wengine waliobadilishwa yaliyomnufaisha Mgumba kwa kupewa unaibu waziri wa Kilimo.

Akizungumza wakati wa kuwaapisha mawaziri hao Julai 3, Rais Magufuli alionyesha kukerwa na wabunge wa CCM waliokuwa wakikosoa suala hilo.

“Nilimwambia Waziri Mkuu kwamba nataka wafanye fujo na ningeanzia kwenye jimbo lake, muulize yuko hapa, kama kuna shangazi zake nitaanza kupiga hao. Lazima tufika mahali tuambizane ukweli,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza: “Na nilimwambia kwamba Mtwara na Lindi kuna wabunge wangapi wa CCM, akasema wako 17... Nikasema niko radhi waondoke wote, tutakuwa bado tuna column ya kuongoza nchi. Nikawa nimempigia na Katibu mkuu wa CCM tukae kwenye mpango huo.”

Aliendelea; “Nataka niwaeleze ukweli, nilimweleza saa nane za usiku, pamoja na yeye angeondoka, si na yeye ni mbunge wa huko wanaohusika na hili zao?”

Baadaye, Ghasia aliyekuwa pia mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, na makamu wake, Jitu Soni walitangaza kujiuzulu nafasi zao bila kueleza sababu zozote.

Mzozo mpya

Kama wasemavyo Waswahili, ‘La kuvunda halina ubani’ ndivyo ilivyotokea, sasa soko la korosho limeingia mzozo baada ya bei yake kushuka katika soko la dunia.

Tofauti na mwaka jana ambapo wakulima waliuza hadi Sh4000 kwa kilo, mwaka huu wafanyabiashara wamekuja na bei ya Sh2,700 na hata Serikali ilipozungumza nao waliishia kununua kwa bei ya Sh3,000.

Hapo ndipo, Rais Magufuli alipotangaza kuwaunga mkono wakulima waliogoma kuuza korosho zao, huku akifanya mabadiliko ya mawaziri kwa kumtoa aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na kumweka Japhet Hasunga, pia akimtoa aliyekuwa waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na kumweka Joseph Kakunda.

Rais Magufuli pia amelipa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kazi ya kusimamia na kusafirisha korosho.

Je, hatua hiyo itairudisha korosho palipotakiwa?

Alipoulizwa kwa simu kuhusu maoni kwa sakata hilo mpaka lilipofikia, Nape alisema; “Sitaki kuzungumzia masuala ya korosho kwa sasa.”


Advertisement