Seif aizushia jambo CCM

Naibu Katibu Kkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na wanachama wa chama hicho katika eneo la Magomeni mjini Unguja wakati wa mwendelezo wa ziara maalumu ya kichama yenye lengo la uhamasishaji wa chama. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

Katiba inaeleza bayana kuwa Tanzania ni nchi moja inayotawaliwa na Serikali mbili

Unguja. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema wamebaini dhamira ya CCM kutaka kuifanya Tanzania yenye Serikali moja itakayoongoza Zanzibar na Tanzania bara.

Maalim Seif aliyasema hayo juzi akizungumza na wanachama wa CUF katika ofisi ya Kilimahewa mjini hapa.

Akizungumzia madai hayo, katibu wa uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao alikanusha madai hayo na akidai hiyo si ajenda ya chama chao na hawajawahi kufikiria suala hilo.

Maalim Seif alisema wanaamini mikakati inayoendelea kupangwa na kuratibiwa ikiwamo ya kununua wabunge inalenga kuifanya Tanzania kuwa na Serikali moja.

Akifafanua zaidi hata hivyo Maalim Seif alisema suala hilo haliwezi kukubalika kwa sababu Serikali ya Zanzibar ipo kwa mujibu wa katiba hivyo kuifuta ni kuivunja katiba.

Kuhusu migogoro iliyopo kwenye chama chao, alisema wanachama wamejiandaa na matokeo yoyote yatakayotolewa na Mahakama na kwamba, iwapo watashindwa haitakuwa mwisho wa harakati za kisiasa kwa upande wao.

Naye Catherine alisema kila kitu kinaendeshwa kwa misingi ya kikatiba na ilani ya CCM, hivyo suala hilo halimo katika pande zote hizo.

Catherine alisema kila mtu anafahamu katiba imeweka wazi uwapo wa Serikali mbili kwenye nchi moja na kila moja inafanya kazi kwa mujibu wa katiba. “Hakuna sehemu yoyote kwenye katiba ya chama wala nchi inayoonyesha kuwa CCM ina ajenda ya kuleta Serikali moja Tanzania,’’ alisema.