Sera na sheria mpya zitakavyokibadili kilimo

Muktasari:

Neno “kilimo cha matamko” ni rahisi kuingia kichwani baada ya kusikia mjadala mpana unaohusu jinsi ambavyo kilimo kimekuwa kinashughulikiwa kwa miaka mingi hapa nchini.

Neno “kilimo cha matamko” ni rahisi kuingia kichwani baada ya kusikia mjadala mpana unaohusu jinsi ambavyo kilimo kimekuwa kinashughulikiwa kwa miaka mingi hapa nchini.

Kwa miaka mingi tangu uhuru bila shaka hakuna ambaye hajasikia kauli kama kilimo ni ‘uti wa mgongo’, ‘kilimo cha kufa na kupona’, ‘siasa ni kilimo’, ‘kilimo kwanza’ na nyinginezo zinazoonyesha kwamba kilimo ni cha muhimu hapa nchini.

Hata hivyo, kama kuna juhudi zimefanyika katika kukipa kilimo kipaumbele, zitakuwa ni kidogo ambazo hazijaonyesha tija kubwa.

Hata katika mjadala wa Jukwaa la Fikra linaloendeshwa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) juzi usiku, hali hiyo ilijionyesha wazi. Ndio kisa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akasema “kilio chenu kimesikika”.

Waziri akasema katika kuhakikisha Serikali inawafikia wakulima na kumaliza kilio chao cha muda mrefu, itafanya mabadiliko ya sera na kuandaa upya sheria zake ili kilimo kiweze kuleta tija.

Katika mjadala huo ambao kaulimbiu ilikuwa kilimo maisha yetu, Hasunga anasema kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kinachosemwa ndicho kinachofanyika.

Kabla ya mjadala huo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa ajibu maswali ya wabunge Bungeni akisema Serikali inakwenda kuondoa tozo zote sumbufu kwenye sekta ya kilimo ikiwamo pembejeo ili kuhakikisha wakulima wanazipata kwa wakati na kuboresha sekta hiyo.

“Lengo ni kuhakikisha kunakuwa na kilimo chenye tija badala ya cha mazoea. Kwa kulitambua hilo tutaondoa tozo zote zinazoikwamisha sekta hiyo na nyingine ikiwamo za biashara,” anasema Majaliwa.

Majaliwa alikuwa akijibu swali la mbunge wa Madaba, Kizito Mhagama ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kupunguza tozo kwa maduka yanayouza pembejeo ili kumwezesha mkulima kuzipata kwa gharama nafuu.

Majaliwa anakiri kupokea imepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wakiwamo na wauzaji wa pembejeo juu ya tozo mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli nzima wa biashara zao.

“Serikali imesikia vilio vyenu na sasa inafanya mapitio ya tozo hizo na itakapofikia hatua nzuri itawajulisha na kuwashirikisha kujua ni aina gani ya tozo ambazo zitaondolewa au kuzibadilisha ili mwendelee kufanya biashara zenu katika mazingira rahisi, ”anasema Majaliwa.

Pengine hilo la tozo ni moja ya mambo ambayo Hasunga anazungumzia kuhusu kubadili kanuni na sheria, lakini yeye anazama zaidi akiibua kiini cha kilimo kutokuwa na tija kwa miaka mingi.

Hasunga anasema kuwa kauli za tangu uhuru kama kilimo cha kufa na kupona, kilimo kwanza na kilimo kabambe hazijakisaidia, kimeendelea kuwa nyuma.

Ingawa hata hizo kauli za awali ziliambatana na mabadiliko ya sera, pengine hii ya sasa inaweza kutoa mwanga zaidi kwa kuwa anasema itaambatana na mabadiliko ya sheria.

Kwa mujibu wa Hasunga, sera ya kilimo imekuwapo tangu mwaka 2013 lakini haikuwa na sheria yake, hivyo watafanya mabadiliko ya sera hiyo sambamba na kutengeneza sheria yake.

Anasema huo ni mkakati wa kuandaa chakula cha miaka 100 ijayo kwa kuwa watanzania watakuwa wameongezeka hadi milioni 300 badala ya kusubiri hadi kufikia huko.

Kama walivyowahi kusema viongozi wengine wa miaka ya nyuma, Hasunga anawataka wananchi kutambua kuwa kilimo ndiyo kila kitu, hivyo kutafakari namna sahihi ya kukiinua.

“Tujitafakari kwa pamoja tunakosea wapi na kukiacha kilimo kikiwa chini licha ya mipango na kauli mbalimbali ambazo zimekuwapo huko nyuma. Maboresho ya sera na sheria ya kilimo vitakuwa na nguvu iwapo kila mmoja atakuwa na nia ya dhati ya kukiinua,” anasema.

Licha ya umuhimu wake, nani anakijua kilimo? Mtafiti mshauri wa uchumi wa kilimo kutoka Chuo cha Kilimo (Sua), Dk Anna Temu anasema elimu ya kilimo imefika mbali, lakini bado kuna vijana wengi wanaachwa, hawapati.

“Kunatakiwa kuwe na elimu ya ujasiriamali na mabadiliko katika sekta ya kilimo. Hii ni pamoja na kuongeza ujuzi ikiwamo teknolojia.

Hata hivyo, teknolojia katika kilimo si rahisi kuwafikia watu kutokana na gharama zake, japokuwa zipo huduma za kifedha kwa wale wenye uwezo wa kuzifikia.

Japhet Justine ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) anathibitisha kuwa upo uwezekano wa kupata mikopo katika benki hiyo ili kukata kiu ya wakulima.

Anasema kuna fursa ya kuongeza thamani katika kilimo kwa sababu mazao ya kilimo yanatumika kwa asilimia 65 ya malighafi zinazotoka kwenye kilimo.

“Hii ni fursa, na benki ya kilimo ipo tayari kusaidia hilo, wanaotaka kujenga viwanda vya kufanya kazi hiyo sisi tupo tayari kuwakopesha,” anasema.

Waziri Hasunga anakubaliana na jambo hili. Anasema kwa mwaka 2017, sekta ya kilimo ilitengeneza asilimia 65.5 ya ajira za moja kwa moja kwa Watanzania pamoja na asilimia 10 ya Watanzania wengine wanaofanya biashara za kilimo. Kilimo chenyewe kilichangia asilimia 28.7 kwenye Pato la taifa. Pia, karibu asilimia 70 ya ardhi ya ukulima wa mazao inalimwa kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 kwa kutumia maksai na asilimia10 kwa kutumia trekta.

Nini kifanyike?

Waziri anasema yanahitajika mapinduzi ya sekta ya kilimo kama zilivyofanya nchi nyingine.

Anasema kuwa kilimo ndiyo eneo pekee lenye ajira isiyohitaji mahojiano, bali unajihoji mwenyewe unataka kulima nini, utauza wapi na utamuuzia nani.

Anabainisha fursa nyingi zilizopo katika sekta ya kilimo ikiwamo uzalishaji wa sukari, mafuta ya aina mbalimbali na zao la kokoa ambalo kitaifa linazalishwa tani 19, 910.