Serikali ina imani na Barrick, Acacia yatoa msimamo

Muktasari:

  • Serikali imesema bado ina matumaini na makubaliano yaliyofikiwa kati yake na kampuni ya Barrick Gold Corparations, licha ya taarifa zinazoeleza kuwa kampuni ya uchimbaji wa madini ya Acacia haikubaliani

Dar es Salaam. Serikali imesema bado ina matumaini na makubaliano yaliyofikiwa kati yake na kampuni ya Barrick Gold Corparations, licha ya taarifa zinazoeleza kuwa kampuni ya uchimbaji wa madini ya Acacia haikubaliani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Barrick, Mark Bristow alieleza juu ya taharuki inayotokana na kampuni ya Acacia kutokubaliana na mwafaka uliopatikana katika mazungumzo hayo na kupendekeza kuwa, pengine Barrick itafanya shinikizo ili kupata hatima ya biashara yao hapa nchini. Hata hivyo, hakusema hilo litafanyika lini.

Acacia ndiyo kampuni kubwa ya uchimbaji madini hapa nchini ambayo ina miliki migodi ya North Mara, Bulyankuru na Pangea (Buzwagi), Barrick ina miliki asilimia 64 ya hisa katika migodi hiyo. 

Acacia ambayo ni wazalishaji wakubwa wa dhahabu ikiwa imeorodhesha katika soko la hisa la Landon, imekuwa katika mgogoro na Serikali ya Tanzania tangu Julai 2017 baada ya kupewa madai ya Dola 190 bilioni za Marekani kwa kile kilichoelezwa kuwa haikuwa ikiweka bayana kiasi halisi cha madini yaliyokuwa yakisafirishwa.

Bristow ambaye amekamata nyadhifa ya kuiongoza kampuni hiyo Januari mwaka huu amekuwa na hamu kubwa ya kumaliza mvutano huo kwa kuingia makubaliano na Serikali, lakini katika mahojiano ya wazi alibainisha taharuki iliyopo kuwa Acacia haionyeshi nia ya kumaliza jambo hilo.

 “Tutafika hatua ya kuingia na kushinikiza kumalizika kwa jambo hili, lakini kwa sasa hiyo sio njia sahihi ya kutatua tatizo hili,” amesema Bristow na kuongeza:

“Katika jambo hili kila suluhisho ni muhimu kuliko kutokuwapo” alinukuliwa na vyombo vya habari katika mahojiano aliyoyafanya juzi jijini Toronto, Canada.

Hata hivyo, Acacia ambayo haijashiriki moja kwa moja katika majadiliano hayo ya Serikali ya Tanzania na Barrick jana ilitoa taarifa iliyosema kuwa itatafuta ufafanuzi kutoka kwa Barrick kuhusiana na maoni yaliyobainishwa hayaendani na kile wanachokifahamu wao.

Hata hivyo, wamesema mpaka sasa hawajapata taarifa rasmi ya mapendekezo yaliyofikiwa na pande mbili (Barrick na Serikali). 

 “Pindi Barrick itakapokuwa tayari kuleta mazungumzo yao katika mwafaka wenye mafanikio na kampuni yetu ikapokea mapendekezo yaliyofikiwa kati ya Serikali na Barrick, kamati huru ya bodi ya Acacia itaamua kama iwapo mapendekezo hayo yatapelekea kwa wabia wa kampuni hiyo kwa ajili ya maamuzi au vingine,” imeeleza taarifa hiyo.

Mamlaka za Tanzania jana zilisema haziwezi kutoa tathmini kamili juu ya msimamo wa taarifa hiyo, lakini kuna imani ya kufikia suluhisho linalofaa.

Katibu mkuu wa tume ya madini nchini, Profesa Shukrani Manya amesema majadiliano yanaendelea na hakuna tarehe ya ukomo iliyowekwa kukamilisha malipo.

 “Bado tunaendelea na majadiliano na Barrick, iwapo wataamua kutulipa mapema hilo ni jambo jema kwetu,” amelieleza gazeti dada la The citizen wakati wa mahojiano katika simu.

Alipotafutwa Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema yupo Dar es Salaam kwa shughuli za kikazi na ataweza kutoa maoni juu ya jambo hili baada ya kuwashirikisha wajumbe wa timu ya majadiliano jijini Dodoma.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye ndiye anayeongoza timu ya majadiliano, Profesa Palamagamba Kabudi, alitafutwa katika simu bila mafanikio.

Pia, Barrick na Serikali awali walisema mpango ni kulipa Serikali Dola 300 milioni za Marekani ili kumaliza madai ya kodi na kuwa kutoa ubia wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Serikali na shughuli za Acacia zinazofanyika hapa.

Acacia wamekuwa hawashirikishwi katika majadiliano hayo lakini bodi yake ndiyo itakayopaswa kupitisha majadiliano hayo. Hata hivyo, vyanzo vya ndani vinadokeza kuwa Barrick sasa inataka kuchukua shughuli zote za Acacia nchini kwa asilimia 100 na kuna baadhi ya ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa kuna kampuni za China zimeonyesha nia kufanya biashara hiyo.