Serikali kuanika ushahidi kesi ya Kitilya, wenzake kesho

Muktasari:

  • Kesho Alhamisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kesi mbalimbali za vigogo zitaendelea ikiwamo ya aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kesho Alhamisi Januari 24, 2019  anatarajiwa kuanika wazi ushahidi na mashahidi atakaowatumia katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne, wanaokabiliwa na kesi hizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mbali na kesi ya Kitilya na wenzake, pia DPP kesho anatarajia kuweka wazi ushahidi na mashahidi atakaowatumia katika kesi mbili za uhujumu uchumi zinazomkabili mfanyabiashara aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli, kuwa alikuwa anaiibia Serikali Sh7 milioni kwa dakika, Mohamed Yusufali na wenzake.

DPP anatarajiwa kuweka wazi ushahidi huo pamoja na mashahidi hao kwenye kesi hizo, wakati washtakiwa watakaposomewa maelezo ya mashahidi hao, baada ya upelelezi wa kesi hizo kukamilika.

Mbali na maelezo ya mashahidi na mashahidi hao, pia itaweka wazi vielelezo ambavyo itavitumia katika kesi hizo wakati wa usikilizwaji wa kesi hizo, katika kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Hatua itakuwa inahitimisha jukumu la Mahakama ya Kisutu katika kesi hizo zilizofunguliwa mahakamani hapo kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali, kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa maelezo hayo ya mashahidi, majalada ya kesi hizo yatafungwa rasmi katika mahakama hiyo, kisha kesi hizo zitahamishiwa Mahakama ya Mafisadi kwa ajili kuanza usikilizwaji wa ushahidi, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kisheria kusikilza kesi hizo.

Kesi ya Kitilya na wenzake

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 2 ya mwaka 2019, Kitilya na wenzake kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 58, na mashtaka 49 ni ya utakatishaji fedha, mashtaka matatu ya kughushi na mawili ya kutoa nyaraka za uwongo.

Mashtaka mengine shtaka moja la kuongoza mtandao wa uhalifu, shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu moja lingine la kula njama za kutenda kosa kwa nia ya kumdanganya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.

Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine ni mshindi wa Mashindano ya Urembo (Miss Tanzania), mwaka 1996, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon, ambao walikuwa maafisa wa Benki ya Stanbic.

Wengine ni aliyekuwa Kamishna wa Sera na Madeni Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda (kwa sasa yuko Ofisi ya Waziri Mkuu) na Alfred Misana, ambaye alikuwa Kamishna Msaidizi wa Serana Madeni kutoka wizara hiyo ambaye kwa sasa yuko wizara ya afya.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti tofauti kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi.

Makosa hayo yalitokana na mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingereza, kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4, kupitia kampuni ya Egma T Ltd.

Katika mashtaka hayo wanadaiwa kujipatia Dola za Marekani 6milioni kwa njia za udanganyifu kupitia kampuni ya Enterprises Growth Market Advisors (EGMA) kama ada ya uwezeshaji wa mkopo huo ya asilimia 2.4 na kisha kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Washtakiwa hao watasomewa maelezo ya mashahidi hao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mmbando.

Kesi ya aliyetajwa na Magufuli

Yusufali anakabiliwa na kesi mbili tofauti. Katika kesi ya kwanza, kesi ya uhujumu uchumi namba moja ya mwaka 2019, Yusufali na wenzake wawili wanakabiliwa na mashtaka ya 39 likiwemo kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.9 bilioni.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mmbando ni Alloyscious Gonzaga Mandago na Isaac Wilfred Kasanga na wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 2, 2010 na Aprili 26, 2016 katika maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam ambapo wanadaiwa kula njama kwa kugushi, kukwepa kulipa kodi na kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Katika kesi nyingine namba 4 ya mwaka 2019, Yusufali na mwenzake mmoja Arifal Paliwala, wanakabiliwa na mashtaka 601 ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Sh14.9 bilioni.