Serikali kubadili mfumo wa wadhibiti elimu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (kulia) akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2019/2010, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali imebadili mfumo wa wadhibiti elimu ili kuachana na utaratibu wanaoutia sasa unaosababisha kuwatisha watu

Dodoma.  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali imebadili mfumo wa wadhibiti elimu nchini Tanzania ambao utawawezesha kuondokana na kufanya kazi kwa mfumo wa kipolisi.

Ndalichako ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 9, 2019 wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2019/2020.

Amesema Serikali iko makini katika udhibiti ubora wa shule kwa sababu wanaamini ndio jicho lake kwa kuhakikisha wanafikia malengo.

Amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuangalia kwa umakini idara hiyo na bajeti ya mwaka jana wametoa magari 45 kwa ajili ya udhibiti pamoja na kompyuta.

“Tumeangalia wadhibiti ubora wamekaa kipolisi wanawatisha badala ya support (kusaidia). Tumetengeneza kihunzi bora, ”amesema.

Pia amesema watahakikisha maabara 1,696  zinazojengwa na wananchi zinapata vifaa vya kufundishia kuanzia kidato cha kwanza hadi sita.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema wizara hiyo imejipanga kuhakikisha inainua kipato cha Mtanzania kupitia mifugo na uvuvi na kuwa na mchango mpana katika pato la Taifa.

“Tumeweka mikakati, kwanza kudhibiti mnyororo wa thamani kuanzia kumuandaa ng’ombe hadi kumchakata, kuna viwanda Pwani, Morogoro na tupo katika maridhiano na Serikali ya Misri na tutakuwa na kiwanda pale Ruvu,” amesema Ulega.