Serikali kuikatia rufaa hukumu ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi

Muktasari:

Siku kadhaa baada ya Mahakama Kuu kutoa hukumu iliyozuia wakurugenzi kusimamia uchaguzi, Serikali imekata rufaa kupinga uamuzi huo

Dar es Salaam. Serikali imeamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia Wakurugenzi (DEDs) kusimamia uchaguzi.

Uamuzi huo wa Serikali umebainishwa leo Jumatatu, Mei 13, 2019 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Aderladus Kilangi, wakati akizungumza na wanahabari kutoa msimamo wa Serikali kuhusu hukumu hiyo ya Mahakama Kuu.

Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu, Dk. Atuganile Ngwala, Dk Benhajj Masoud na Firmin Matogolo ilibatilisha kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Pia ilibatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

Katika hukumu hiyo mahakama hiyo ilisema kwamba vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi ikibainisha kuwa wakurugenzi hao huteuliwa na Rais aliyeko madarakani ambaye hutokana na chama tawala na kwamba wengine ni wanachama wa chama cha mamlaka inayowateua jambo ambalo huathiri utendaji wao katika kutenda haki.

Pia ilisema kwamba sheria haijaweka ulinzi kwa NEC kumteua mtumishi yeyote wa umma kuhakikisha kuwa anakuwa huru katika kutekeleza majukumu yake.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu umetokana na kesi iliyofunguliwa na mashirika kadhaa ya wanaharakati kupitia kwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, akitetewa na Wakili Fatma Karume.

Lakini leo AG. Dk Kilangi amesema kwamba tayari Serikali kupitia kwa Wakili Mkuu wa Serikali (SG) imewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

"Pia tumeshaomba nakala ya hukumu pamoja na kumbukumbu za mwenendo wa kesi," ameongeza Profesa Kilangi.

Profesa Kilangi amesema kuwa hata hivyo kuwepo kwa hukumu hiyo hakutaweza kuathiri chaguzi nyingine zijazo zikiwemo za marudio, kwani baada tu ya kuwasilisha taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa utekelezaji wa hukumu hiyo husimama, hadi pale rufaa ya Serikali itakapoamriwa.