Serikali kujenga hospitali ya kikanda ya kitalii Geita

Sunday June 16 2019

 

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

Geita. Wizara ya Afya imetangaza kujenga hospitali ya rufaa ya kikanda mkoani Geita ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma za kibingwa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo Jumapili Juni 16, 2019 katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kitaifa Katoro mkoani Geita.

Waziri Ummy amesema licha ya kuwepo kwa Hospitali ya Bugando Mwanza, Serikali imeona ni vema kujenga hospitali nyingine Geita kutokana na idadi kubwa ya wananchi.

Amesema Kanda ya Ziwa inakadiriwa kuwa na watu 13.4 milioni.

Waziri Ummy amesema hospitali hiyo itakuwa kituo cha utalii cha matibabu kwa nchi jirani za Congo, Rwanda na Burundi .

Aidha, ametangaza kujengwa kwa hospitali nyingine wilayani Geita katika Jimbo la Busanda kutokana na idadi kubwa ya watu wilayani humo.

Advertisement

Tayari ujenzi wa hospitali hiyo unaendelea katika jimbo la Nzera na Waziri Ummy ameahidi wizara itatoa Sh500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali nyingine ya wilaya itakayojengwa Katoro.

Advertisement