Serikali kujenga kitengo cha watoto JKCI

Muktasari:

  • Serikali imeidhinisha Sh500 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kitengo cha watoto kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) uliogharimu Sh2 bilioni.

Dar es Salaam. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  imewekeza kiasi cha Sh1.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kitengo cha watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Kujengwa kwa kitengo hicho kutaiwezesha JKCI kuwafanyia upasuaji wa kufungua vifua watoto 40 kwa mwezi kutoka 20 wa hapo awali pamoja na vyumba vinne vya madaktari wa kuona wagonjwa watoto wanaougua maradhi hayo kutoka kimoja cha awali.

Akizungumza baada ya ukaguzi wa kitengo hicho leo Jumapili Januari 20, 2019 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Rais Magufuli tayari ameidhinisha Sh500 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo ifikapo Januari 28, 2019.

Amesema kitengo hicho kinachotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, kimegharimu Sh2 bilioni ambazo fedha nyingine Sh800 milioni zimetolewa na wafadhili Charity Baptism.

“Serikali awali iliweka Sh700 milioni na wiki hii mheshimiwa Rais ametoa Sh500 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi ili watoto wahamie katika jengo hili,” amesema Waziri Ummy.

Ummy amesema mwaka 2018 JKCI ilifanya operesheni nyingi zaidi kwa watoto hivyo anategemea mwaka huu zitaongezeka zaidi, “Hii itakuwa wodi ya kwanza kwa ajili ya watoto pekee kwa Afrika Mashariki walio wengi wanachanganya watoto na wakubwa.”

Katika ukaguzi huo, Waziri Ummy ametoa maelekezo mbalimbali ya maboresho ya wodi hiyo inayotarajiwa kukabidhiwa ifikapo Januari 28 mwaka huu.

Mkurugenzi mtendaji JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema kitengo hicho kipya kilichoanzishwa pembeni mwa jengo hilo kitakuwa na vitanda 32 kutoka 11 vya awali.

“Watoto walikuwa na vitanda 11 pekee lakini kwa sasa tutakuwa navyo 32 na vitanda vya ICU vitakuwa 15,” amesema Profesa Janabi.