Serikali ya Kenya yamtaka Jaguar awaombe wananchi msamaha

Muktasari:

  • Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Kenya, Dk Fred Matiangi amemtaka Mbunge wa Starehe, Charles Kanyi maarufu Jaguar kuwaomba wananchi msamaha kutokana na kutoa kauli za chuki dhidi ya wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda waliopo jijini Nairobi.

Dar es Salaam. Serikali ya Kenya imemtaka Mbunge wa Starehe, Charles Kanyi maarufu Jaguar kuwaomba wananchi msamaha kutokana na kuwadhalilisha kwa kutoa kauli za chuki dhidi ya wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda waliopo jijini Nairobi.

Waziri wa Usalama wa Ndani nchini humo, Dk Fred Matiangi amesema kuwa Jaguar anapaswa kuwaomba wananchi msamaha kwani hakuna sera ya Serikali ya Kenya inayoruhusu kuwatenga na kuwanyanyasa wageni hasa majirani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema kama kungekuwa na shida mbunge huyo angewasiliana na vyombo vinavyohusika vikiwemo vyombo vya usalama na viongozi wa bunge.

“Huwezi kuchukua sheria kwa mikono yako eti uwe unaanza kuwaambia watu utawafukuza, utawapiga. Hakuna mtu atapigwa hapa, alichofanya mbunge huyo ni aibu na ni udhalilishaji kwa nchi. Inabidi aombe msamaha sio kwa sisi Serikali lakini kwa wananchi wa Kenya kwa kutudhalilisha sisi wote” amesema Matiangi

Amesema lengo la Kenya ni kuendeleza mshikamano kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuhakisha usalama wa wananchi hivyo matamshi ya mbunge huyo yanaweza kuleta shida.

“Sisi tunazingatia maagano tuliyokuwa na wenzetu katika nchi jirani kwamba tutaanza sasa mpango wa kuishi kama ndugu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, sisi kama viongozi hatuwezi kuzungumza maneno kama yale yaliyokuwa yanazungumziwa na mwenzenu wakati ule,” amesema na kuongeza

“Lazima tuhakikishe kuwa tunalinda wananchi, kwa sababu mtu mwingine naye akisikia hivyo, aanze kusukuma Wakenya sehemu wanafanya biashara, itatuletea shida,” amesema

Siku za hivi karibuni, Jaguar alitoa kauli za chuki dhidi ya wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda waliopo jijini Nairobi akisema wakamatwe na kupigwa.