Serikali ya Kenya yazungumzia kauli ya Jaguar

Muktasari:

  • Mbunge wa Starehe nchini Kenya, Charles Njagua Kanyi maarufu Jaguar jana alitoa saa 24 kwa raia wa kigeni waliopo nchini humo, wakiwemo Watanzania kurejea makwao na ikiwa hawatafanya hivyo, wananchi wa Kenya watavamia maeneo yao, yakiwemo ya biashara. Hata hivyo Serikali ya Kenya imekana kuhusika na kauli hiyo.

Dar es Salaam. Serikali ya Kenya imewahakikishia wafanyabiashara wa kigeni nchini humo usalama wakati wote huku ikisema Serikali haipo upande wa Mbunge wa Starehe, Charles Njagua maarufu Jaguar kuhusu kauli alizozitoa.

Mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki kupitia mitandao ya kijamii jana Jumanne ilisambaa video yake akieleza kuwafukuza wafanyabiashara wa kigeni wakiwemo Watanzania ndani ya masaa 24 kurudi kwao la sivyo watawapiga na kuwarudisha nchini mwao.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne Juni 25, 2019 na Msemaji wa Serikali ya Kenya, Cyrus Oguna imelaani kauli ya Jaguar na kueleza haikubaliki katika kipindi hiki cha utandawazi.

“Wakenya ni watu wenye upendo na amani ambao kwa miaka mingi wameshirikiana na mataifa mbalimbali. Hii ni tunu tunajivunia na tutaendelea kushirikiana,” imeeleza taarifa.

Oguna amesisitiza usalama wa mali na watu kutoka mataifa mbalimbali pindi watakapo wekeza katika nchi hiyo utaendelea kama ulivyo sasa.

Mapema jana kupitia mtandao wa Twitter @RealJaguarKenya alitolea ufafanuzi kuwa kauli aliyotoa ililenga raia wa China waliovamia biashara za Wakenya.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu kauli hiyo ya Jaguar, kiongozi huyo aliwatoa hofu Watanzania baada ya kusema wamewasiliana na Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania ambao ulisisitiza Serikali kutohusika na maneno ya Jaguar.