Serikali ya Tanzania kuimarisha miundombinu chuo cha kijeshi Duluti

Maafisa Wakuu wa kijeshi waliohitimu mafunzo yao katika Chuo cha Ukamanda na Unadhimu ,Duluti wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha , kati yao wametoka katika nchi sita za Afrika .Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya Chuo cha Kijeshi cha Ukamanda na Unadhimu, Duluti  ili kiweze kutoa mafunzo zaidi kwa maofisa wakuu wa ndani na nje ya nchi.

Arusha. Serikali imesema itaendelea kuboresha miundombinu ya Chuo cha  kijeshi cha ukamanda na unadhimu (CSC) kilichopo eneo la Duluti wilayani Arumeru, ili kiwe na hadhi ya kimataifa.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi  alipokuwa akizungumza jana Jumamosi Juni 22, 2019 katika mahafali ya 33 ya Chuo  hicho  kinachotoa mafunzo ya miaka miwili kwa maofisa wakuu wa jeshi.

Dk Mwinyi amesema Serikali inatambua umuhimu wa mafunzo yanayotolewa na itaendelea kukiimarisha hatua kwa hatua.

Amesema lengo la kuwa na chuo hicho ni kuwapa maarifa ya juu ya kijeshi na kiraia maofisa hao kwa ajili ya kuwa na utayari wa kuongoza maofisa na askari walio chini yao kwenye mapambano ya kivita pindi yakitokea lakini pia kuihudumia jamii inayowazunguka mara baada ya utumishi jeshini.

 

Dk Mwinyi amesema ushirikiano wa Tanzania na nchi za Afrika Mashariki (EAC)  na za Kusini mwa Afrika( SADC) utaendelea kuimarishwa.

“Tumekua na ushirikiano na nchi hizo katika nyanja mbalimbali zikiwemo za mafunzo ya kijeshi kama mlivyoshuhudia wapo maafisa wanafunzi waliohitimu kutoka nchi sita rafiki ,lakini sio wanafunzi tu, pia tumekua na utaratibu wa kubadilishana wakufunzi jambo ambalo linatufanya kuwa na mazingira rafiki ya kuaminiana na ulinzi wa pamoja,” alisema Dk Mwinyi.

Mkuu wa Chuo hicho, Brigedia Jenerali, Ibrahim  Mhona alisema jumla ya maaofisa  wanafunzi 60 wamehitimu na kutunukiwa vyeti kati yao, 13 wametoka Rwanda, Burundi, Uganda, Msumbiji, Zimbabwe  na  Eswatini.

Naye Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dk Eliamani Sedoyeka ambaye Chuo chake a na Jeshi kutoa kozi ya masomo ya Kimkakati (Strategy Studies), amesema wataendelea kushirikiana kwa kufungua wigo zaidi wa kutoa mafunzo ya utafiti, ubunifu na usalama wa kimtandao.