Serikali ya Tanzania yabainisha mabilioni inayodaiwa na walimu

Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Serikali imesema madai ya walimu ya malimbikizo ya mishahara na likizo yanafikia Sh43 bilioni.

Dodoma.  Serikali ya Tanzania imesema hadi sasa walimu wanaidai zaidi ya Sh43 bilioni  yakiwamo malimbikizo ya mishahara na likizo.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amesema leo bungeni Jumatatu Aprili 15, 2019 akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Kiza Mayeye (CUF).

Mbunge huyo amesema walimu wamekuwa hawalipwi fedha za likizo na matibabu licha ya kuwa jambo hilo ni takwa la kisheria kwa mujibu wa kazi.

“Je, ni lini watapewa fedha hizo kwa wakati ili kujikimu pindi wanapokuwa likizo, wanapoumwa wapate nauli kwenda kupata matibabu?” amehoji.

Akijibu swali hilo, Waitara amesema Serikali ina nia nzuri kuhakikisha inalipa walimu kwa wakati na kwamba wapo walimu 86,000 ambao wanaidai Serikali zaidi ya Sh 43 bilioni.

Awali, katika swali lake la msingi mbunge huyo amesema Serikali imekuwa ikiwapandisha madaraja walimu lakini haitoi malipo stahiki kwa madaraja hayo mapya kwa kipindi kirefu tangu walipopanda madaraja yao.

“Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba walimu wanapata stahiki zao mara wanapopandishwa daraja la kazi zao,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Waitara amefafanua kuwa Serikali ilisitisha kupandisha walimu na watumishi wengine madaraja katika mwaka wa fedha 2015/16 na 2016/17 kutokaana na uhakiki wa watumishi uliohusisha uhalali, elimu na ngazi za mishahara.

Amesema lengo la uhakiki lilikuwa ni kuhakikisha kuwa Serikali inabaki na watumishi wenye sifa na wanaostahili kulipwa mishahara.

Waitara amesema kutokana na sababu hiyo ni kweli wapo watumishi ambao walipandishwa madaraja hawajalipwa mishahara mipya, wapo waliopata mishahara mipya na baadaye kuendolewa na wengine hawakupandishwa licha ya kuwa na sifa.

Amebainisha ili kurekebisha changamoto hizo, Serikali ilitoa maelekezo kuanzia Novemba 2017 kwa waajiri wote wakiwamo wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kuhuisha barua za kuwapandisha madaraja watumishi hao ili waweze kulipwa stahili zao.

Amesema kwa ambao walikuwa na barua lakini taarifa zao hazijaingizwa kwenye mfumo, waaajiri walielekezwa kuhuisha barua zao kuanzia Aprili mosi mwaka huu ili waanze kulipwa.

Amesema Serikali inaendelea kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha watumishi wenye sifa ya kupanda madaraja wanalipwa stahili zao.