Serikali ya Tanzania yaeleza mkakati wake kuhamasisha ufugaji nyuki

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema ipo mbioni kuja na mpango mkakati wa kitaifa wa kutoa hamasa kwa wananchi kutambua umuhimu wa kufuga nyuki na faida ya asali kiuchumi na kiafya

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema ipo mbioni kuja na mpango mkakati wa kitaifa wa kutoa hamasa kwa wananchi kutambua umuhimu wa kufuga nyuki na faida ya asali kiuchumi na kiafya.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 20, 2019 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla katika maadhimisho ya siku ya nyuki duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dodoma.

Dk Kigwangalla amesema lengo ni kuwasaidia wananchi wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki kuchakata na kusindika asali kwa pamoja ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.

“Lengo la kuanzisha mpango huo wa kitaifa ni  kuwaenzi nyuki kwa kuwekeza fedha ya Serikali na ujuzi kutoka kwa wataalam. Kwa wananchi ni kuunda ushirika kwa mikoa kumi ya Tanzania Bara, na kila wilaya kuwapa mizinga ambayo wataitumia kwa ajili kufuga nyuki,” amesema Dk Kigwangalla.

Amebainisha kuwa baada ya hapo kila wilaya itakuwa na ushirika na kiwanda kimoja kitakachokuwa kinachakata na kusindika asali.

Amesema mradi huo upo katika hatua nzuri na wameshatenga bajeti ikipita watakuwa na uhakika wa kujenga viwanda kumi kwa kuanzia.

Mikoa ambayo mradi huo utaanzani Katavi, Tabora, Rukwa, Dodoma, Singida, Geita, Kagera na Mbeya.

Maonyesho ya siku ya nyuki duniani yenye kauli mbiu ya ‘Tuwalinde nyuki’ yamefanyika kwa mara ya kwanza leo mkoani Dodoma.