Serikali ya Tanzania yakopa Dola 300 milioni kukarabati reli ya kati

, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwele 

Muktasari:

  • Serikali imekopa zaidi ya Dola 300 milioni kutoka Benki ya Dunia zitakazotumika katika ukarabati wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka.

Dar es Salaam.  Serikali imepata mkopo wa zaidi ya Dola 300 milioni (zaidi ya Sh660 bilioni) kutoka Benki ya Dunia zitakazotumika kukarabati wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ghati namba moja katika Bandari ya Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Isack Kamwele amesema mradi huo utakamilika Juni 2020 hatua hivyo kuongeza idadi ya watumiaji wa bandari hiyo.

Amesema reli hiyo ya kati ambayo ilijengwa na Ujerumani mwaka 1902, iliruhusu treni kutembea kwa kasi ya kilometa 75 kwa saa uwezo huo ulipungua hadi kati ya kilometa 25 hadi 30 kwa saa.

“Baada ya kukamilika kwa ukarabati huu itarejesha uwezo wake wa kutembea kilometa 75 kwa saa na kubeba tani milioni tano kwa mwaka. Wafanyabiashara wengi watakuja Bandari ya Dar es Salaam kutoka Mwanza hadi Uganda kwa hiyo mizigo itakuwa inaingia Kampala,” amesema Kamwele.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ujenzi wa ghati hiyo ulikamilika Novemba mwaka jana na ni miongoni mwa maghati manane yanayojengwa kwa gharama ya Sh968 bilioni baada ya Serikali kupata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Uingereza.