Serikali ya Tanzania yapokea mabilioni kuhamasisha upandaji miti

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James

Muktasari:

Fedha hizo, Sh24 bilioni ni kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya programu ya "Panda Miti Kibiashara" itakayotekelezwa katika mikoa ya nyanda za juu kusini kwa msaada wa Serikali ya Finland.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imepokea msaada wa Sh24 bilioni (Euro 9.4 milioni) kutoka Serikali ya Finland kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya programu ya "Panda Miti Kibiashara."

Programu hiyo itatekelezwa katika mikoa ya nyanda za juu kusini ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Morogoro ambapo wakulima watajengewa uwezo wa kupanda miti na kunufaika na miti hiyo baada ya muda fulani.

Akizungumza leo Alhamisi Julai 18,2019 baada ya kutiliana saini mkataba wa msaada huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amesema utekelezaji wa programu hiyo utachangia kufikiwa kwa malengo ya awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano kwa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi unaowafikia wananchi wengi.

"Hakika programu hii itasaidia kuongeza mashamba ya misitu itakayoleta faida za kijamii, kimazingira na kifedha katika maeneo ya mradi," amesema James.

Katika awamu ya kwanza iliyotekelezwa kati ya mwaka 2014 na 2018, amesema Serikali ilipokea msaada Sh49.8 bilioni ambazo zimeleta mabadiliko makubwa hapa nchini katika sekta mbalimbali.

Amesema katika awamu ya pili ya programu hiyo, shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo kuimarisha vikundi vya wapandaji miti kwa kuviwezesha kupata usajili, kuwajengea uwezo wadau wote wa misitu kupitia upandaji miti, kuongeza uwezo na rasilimali za kudhibiti moto katika mashamba ya miti na kuongeza ubora wa mazao ya misitu.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Finland nchini Tanzania, Kari Leppanen amesema Tanzania na Finland zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na uhusiano huo umekuwa ukiimarishwa katika uhifadhi wa mazingira na kuwajengea wananchi uwezo.

Amesema uchumi wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika unategemea misitu, ndiyo maana wameamua kusaidia katika eneo hilo ili wananchi mmoja mmoja waweze kunufaika na upandaji miti wakati huo huo wakihifadhi mazingira yao.

"Lengo ni kuwasaidia wakulima masikini ili waweze kuboresha maisha yao kupitia upandaji miti na kuitumia miti hiyo kufanya biashara itakayowaingizia kipato," amesema kaimu balozi huyo wa Finland.