Serikali ya Tanzania yasema haitapiga magoti kuomba msaada

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imesema kamwe haitampigia mtu magoti kuomba msaada kwa maelezo kuwa imeamua kujitegemea

Dodoma. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Serikali ya Tanzania haitampigia mtu magoti kuomba msaada.

Ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Mei 30, 2019 wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje mwaka 2019/2020.

Amesema Tanzania haikupiga magoti katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Pili licha ya nchi kutokuwa na akiba ya fedha za kigeni, akibainisha kuwa kwa sasa Taifa hilo lina akiba ya fedha za kigeni ya miezi mitano.

"Kama tuliweza kwa wakati huo hatuwezi kushindwa katika awamu hii ya Magufuli (Rais John) tumeamua kujitegemea," amesema Kabudi.

Profesa Kabudi amesema Tanzania ni nchi pekee Afrika ambayo haijawahi kushindwa vita na ndiyo nchi iliyowarudisha wapigania uhuru katika nchi zao.

Profesa Kabudu alitumia neno Mabarakuli, akisema ni vibaraka wanaofanya kazi ya kubeza juhudi za Serikali wanapoona mafanikio.

Alibainisha kuwa kikazo cha sasa ni cha mwisho kwa fedheha na kwamba miaka ijayo hata wajukuu hawatakiwi kuona fedheha hiyo.

Akizungumzia Watanzania waishio nje, amewataka kwenda katika ofisi za balozi za Tanzania katika nchi husika ili wakajiandikishe na kutambuliwa.