Serikali ya Tanzania yatoa msimamo bungeni kuhusu Watanzania kupewa saa 24 kuondoka Kenya

Tuesday June 25 2019

 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Kenya imemkana mbunge wa nchi hiyo, Charles Njagua Kanyi maarufu Jaguar aliyewapa saa 24 Watanzania waishio nchini humo kurejea makwao.

Akizungumza bungeni leo jioni Jumanne Juni 25, 2019 wakati akitoa kauli ya Serikali kuhusu kauli ya mbunge huyo kama alivyotakiwa kufanya hivyo na Spika Job Ndugai, Majaliwa amesema Serikali ya Kenya tayari imemtaka aeleze  alitoa kauli hiyo akiwa analenga nini.

Kabla ya Ndugai kumpa nafasi Majaliwa kutoa maelezo ya Serikali, aliwapa nafasi wabunge kutoa maoni yao ikiwa ni baada ya kudai haoni umuhimu wa Serikali kumjibu mbunge mmoja.

Miongoni mwa waliotoa maoni yao ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Video inayosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii inamuonyesha Jaguar ambaye ni mwanamuziki maarufu ndani na nje ya Kenya, akitoa maagizo hayo huku akiwa amezungukwa na umati wa wananchi waliomshangilia na kusindikiza kila eneo alilopita.

Kauli ya Jaguar iliombewa mwongozo bungeni leo mchana na mbunge wa Rufiji (CCM), Mohammed Mchengerwa aliyetaka kujua kauli ya Serikali, Ndugai kumtaka Majaliwa kutoa kauli ya Serikali.

Advertisement

Alichokisema Majaliwa

“Niwasihi tuwe watulivu na Serikali tumelisikia kuanzia jana na hatujakaa kimya tumelifanyia kazi, hatua ambazo tumezipitia ni kumjua mzungumzaji, ni kiongozi wa eneo moja la Kenya, unajua Kenya wameingia katika mchakato wa mchaguzi na huenda alisema kwa mwelekeo huo.”

“Serikali tunatambua Kenya ni nchi rafiki na jirani zetu hata viongozi wetu wakuu wanazungumza lugha moja na Kenya inapakana na Tanzania katika mpaka mrefu sana,” amesema Majaliwa.

Amesema baada ya kauli hiyo Serikali ya Tanzania imewasiliana na balozi wa Kenya nchini na kuzungumza na balozi wa Tanzania nchini Kenya ili kupata picha ya jinsi kauli hiyo ilivyopokelewa.

“Balozi wa Kenya nchini amekanusha kauli ile kuwa si ya Serikali wala si msimamo wa wananchi wa Kenya ni jambo lake binafsi (la Jaguar),” amesema Majaliwa.

Amesema hata Bunge la Afrika Mashariki (EALA) linaloendelea jijini Arusha, mawaziri na wabunge wamelaani kauli ya Jaguar.

“Serikali ya Kenya wametutaka tuwe watulivu na kumtaka Jaguar kusema kauli hiyo ameipata wapi na alikuwa akimaanisha nini. Sisi Watanzania  maeneo yote tulipo kama tuna ndugu zetu Wakenya tuishi nao vizuri na hatuna chuki nao na wao hawana chuki na sisi.”

Awali, Mbowe amesema jambo hilo si la kupuuza kwa madai kuwa alichokizungumza mbunge huyo ni kitu kizito.

“Nina marafiki Kenya na walinipigia simu na kuniuliza nina maoni gani kwa kauli hizo. Sisi kama Watanzania ambao tumetajwa tunahitaji majibu. Ningeshauri Bunge hili litoke kauli ya kukemea na kulaani kauli ile, itambue hatuna ugomvi na serikali ya Kenya lakini ichukue hatua kwa kauli ambayo inahatarisha mahusiano ya nchi zetu,” amesema Mbowe.

Mbunge wa Buchosa (CCM), Dk Charles Tizeba amesema, “Yule mbunge kauli yake unaweza kuidharau, haya mambo yameshatokea katika nchi za Afrika kwa uchochezi mdogo mdogo na watu wamepoteza maisha.”

“Hapa hatuichukulii kama Serikali ya Kenya kuwa ndio yenye mawazo haya lakini kama nchi (ya Kenya) inaweza kusema haipo nae ni mawazo na kauli zake mwenyewe,” ameongeza

Wabunge wengine waliotoa maoni kuhusu kauli ya Jaguar ni mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu, James Ole Millya (Simanjiro), Livingstone Lusinde (Mtera)

Advertisement