Serikali ya Tanzania yaunda kamati ya mazishi ajali ya moto

Waziri Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenister Mhagama

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imeunda kamati maalum itakayofanya maandalizi ya mazishi kwa watu zaidi ya 60 waliofariki katika ajali ya moto baada ya lori la mafuta kupinduka mkoani Morogoro.

Dar es Salaam. Waziri Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenister Mhagama amesema Serikali imeunda kamati ya wataalamu itakayotambua maiti na majeruhi waliotokana na ajali ya lori la mafuta lililopinduka leo Jumamosi mkoani Morogoro na kulipuka.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la ajali leo Jumamosi Agosti 10, 2019, Waziri Mhagama na walemavu amesema baadhi ya mawaziri watakuwa na vikao mkoani humo kujadili jinsi ya kumaliza msiba huo.

“Kuna timu ambayo imeshaanza kufanya ‘assessment’ (mchanganuo) ya namna ambavyo tutakuwa tunahifadhi hawa wenzetu kwa namna yoyote ile. Kama ni ndugu tujue, lakini wale ambao hawataweza kutambulika kama Serikali ya mkoa tujue tunafanya nini,” amesema Waziri Mhagama.  

“Tumeshakubaliana kwamba tuwe na timu itakayokuwa hapa ili kuwa attend (kuwahudumia) Watanzania wale ambao watakuja kutambua ndugu zao. Kuna timu imeshaundwa na itaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini,” amesema.

Amesema timu hiyo pamoja na mambo mengine itafanya utambuzi wa wagonjwa na kuweka utaratibu wa kila mtu kupata nafasi nzuri ya kutambua maiti.

“Tukimaliza kuzungumza na ninyi tutakwenda kuangalia mahali ambapo maiti zimehifadhiwa na mahali majeruhi walipo. Najua kuna watu wanataka tu kuja kuangalia tukio na wengine wanakuja kuangalia ndugu zao,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe amesema baada ya ajali hiyo, Rais wa Tanzania, John Magufuli aliwaagiza mawaziri wote wanaohusika kufika eneo la ajali ambapo amesema Serikali imetoa helkopta mbili.

 “Kama Serikali tumejipanga, Serikali yote iko hapa na macho yote yako Morogoro. Kama alivyozungumza tumepeana saa moja na nusu kila mtu afanye uchunguzi wake kisha tukirudi tutatoa taarifa,” amesema Kamwelwe.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe amewataka Watanzania kuchangia damu kwa majeruhi kwa kadiri itakavyohitajika.

“Timu yetu ya wataalamu tukishirikiana na wizara ya Afya wako kazini wakichambua wagonjwa. Kimsingi tuliona wananchi 50 waliojitokeza kuchangia damu, wengine waendelee kwa sababu mahitaji ya damu yanategemea hali ya mgonjwa,” amesema Dk Kebwe.  

Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mjini, Mary Chonjo amesema kuanzia kesho Jumapili saa 2 asubuhi watanza kutambua miili na kuwataka wananchi waliojitokeza kutambua ndugu zao kutawanyika.

 

Endelea  kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi