VIDEO: Serikali ya Tanzania yawapoza wenye hofu usajili mpya laini za simu

Muktasari:

Imesema wananchi wasiokuwa na vitambulisho vya uraia watapewa utaratibu maalumu wa kusajili laini zao za simu

Dodoma. Serikali imesema Watanzania wasio na vitambulisho vya uraia watawekewa utaratibu maalumu ili  kusajili laini zao za simu kwa kutumia alama za vidole.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatano Aprili 24, 2019 na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akijibu mwongozo wa mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Felista Bura.

Lugola alitoa ufafanuzi huo baada ya awali majibu ya naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye kutowaridhisha wabunge wengi walioonekana kusimama kutaka maelezo zaidi.

Katika mwongozo wake, Bura amesema baada ya Serikali kutangaza mpango huo wa usajili sharti likiwa lazima mhusika kuwa na vitambulisho vya uraia yameibuka malalamiko kwa watu wasiokuwa na vitambulisho hivyo.

“Kwa kuwa leo inasomwa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Nida (Mamlaka ya Usajili wa Vitambulisho vya Taifa) wapo hapa naomba Serikali itoe majibu kuhusu jambo hili,” amesema Bura.

Pia, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa kina katika jambo hilo kwa maelezo kuwa kasi ya utoaji vitambulisho hivyo kwa sasa si kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

“Ni kweli kuanzia Mei mosi, 2019 kampuni zote za simu zinatakiwa kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole baada ya kujiridhisha na utambuzi wa mtu kupitia kitambulisho cha taifa,” amesema Nditiye na kuongeza:

“Tulianza usajili huu kwa majaribio na sasa tunataka kulifanya rasmi zoezi hili baada ya kujiridhisha taratibu zote zipo sawa. Watu ambao wana namba za vitambulisho wapo milioni 16.”

Hata hivyo, Nditiye amesema litaanza Mei mosi, 2019 na watafanya tathmini Septemba mwaka huu na kubainisha kuwa litamalizika Desemba 31, 2019.

“Baada ya hapo laini ambazo watu watakuwa hawajasajili zitazimwa,” amesema Nditiye na kuamsha zogo bungeni.

Katika ufafanuzi wake Lugola amesema: “Watanzania hawapaswi kuwa na wasiwasi. Nida tulikuwa na lengo la kutambua, kusajili na kutoa vitambulisho milioni 24.5 hayo ndio malengo.

“Lakini mpaka sasa Nida tumefanya utambuzi na usajili wa watu milioni 16. Tulipoona kwamba wenzetu wa TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) wanataka kubadili mfumo wa kubadili simu na kutumia alama za vidole na mwenye kitambulisho ndio atasajiliwa. Nida tuliweka utaratibu.

“Watanzania milioni 16 wamepatiwa NIN (National Identification Number) kwa namba hiyo ndio ataweza kusajili laini yake. Kwa hiyo kibindoni tuna Watanzania milioni 16 wenye sifa za kusajiliwa mpaka sasa na tunaendelea na usajili,” amesema Lugola na kuongeza:

“Pale ambako tutakuwa hatujatimiza usajili Mtanzania anayetakiwa kupata namba ili aweze kusajiliwa simu tutampa utaratibu maana si kosa lake kutosajiliwa