Serikali yapunguza mzigo wa kodi kwa wananchi

Sunday February 10 2019

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi akiwasilisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria mbalimbali namba 2 wa Mwaka 2019 bungeni jijii Dodoma jana.Picha na Anthony Siame 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali imepunguza mzigo wa kodi kwa wakulima wa zabibu, wachimbaji wadogo wa madini na wamiliki wa majengo baada ya kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali.

Unafuu huo unafuatia Bunge kupitisha muswada huo wa Sheria Mbalimbali namba 2 ya mwaka 2019 unaopendekeza marekebisho katika sheria tano.

Sheria zilizofanyiwa marekebisho za ushuru wa bidhaa ni kodi ya mapato, mamlaka ya serikali za mitaa ya utozaji wa kodi ya majengo, madini na kodi ya ongezeko la thamani (Vat).

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi alipendekeza jana kupunguzwa kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye pombe kali inayotengenezwa kwa kutumia zabibu zinazozalishwa nchini.

“Lengo la marekebisho haya ni kuhamasisha viwanda kutumia mvinyo unaozalishwa nchini na hivyo kuinua kilimo cha zao la zabibu,” alisema.

Ushuru huo umepungua kutoka Sh3,415 hadi Sh450 kwa lita moja.

Wachimbaji wadogo

Profesa Kilangi alisema wanapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini katika maeneo mbalimbali ikiwemo kifungu cha tisa, kurekebishwa kwa madhumuni ya kujumuisha cheti cha uthibitisho wa kutodaiwa kodi kama moja ya uhamishaji wa umiliki wa leseni za madini. “Marekebisho hayo yanakusudiwa kuhakikisha kwamba kodi zinazohusu leseni za madini zinalipwa kabla ya leseni hizo kuhamishiwa katika umiliki mwingine,” alisema.

Alisema kifungu cha 18 kinarekebishwa kwa madhumuni ya kuweka ukomo wa chini wa adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya madini kinyume cha sheria.

Profesa Kilangi alisema marekebisho ya kifungu cha 27 (C ) yanalenga kuweka ulazima wa ununuzi na uuzaji wa madini kufanywa katika masoko ya madini isipokuwa kwa wamiliki wa leseni kubwa na za kati.

Alisema marekebisho hayo yanapendekeza vituo vya ununuzi wa madini vianzishwe katika maeneo ambayo hakuna masoko ya madini.

“Marekebisho hayo yanategemewa kuweka mfumo madhubuti utakaowezesha wachimbaji wadogo kuuza madini yao.”

Kodi ya Vat

Vilevile Profesa Kilangi alipendekeza kurekebishwa kwa sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kifungu cha 55B.

Alisema marekebisho hayo yanalenga kutoza Vat kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye madini ya metali na vito yatakayouzwa na wachimbaji wadogo wa madini kwenye masoko ya madini.

Alisema lengo la mapendekezo hayo ni kuwahamasisha wachimbaji wadogo kuuza madini yao katika masoko ya madini na kudhibiti utoroshwaji wa madini.

Profesa Kilangi pia alipendekeza kufanyika marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mapato kwa kufuta kifungu cha 83B na aya 4(d).

Alisema lengo la marekebisho hayo ni kuondoa kodi ya zuio ya asilimia tano kwa wachimbaji wadogo wa madini ili kuhamasisha wachimbaji wadogo kuuza madini yao katika masoko ya madini.

Kodi ya Majengo

Kuhusu kodi ya majengo, Profesa Kilangi alipendekeza kufanyiwa marekebisho vifungu vya 6,16,18A,29 na kufuta vifungu vya 18,19,20 na 22 ya Sheria ya Serikali za Mitaa ya utozaji wa Kodi ya Majengo.

Alipendekeza marekebisho ya viwango vya kodi ya majengo ya kawaida kuwa Sh10,000 kwa majengo ya mijini na vijijini.

Profesa Kilangi alisema Serikali inapendekeza marekebisho ya sheria ya serikali za mitaa ya utozaji wa kodi ya majengo lengo likiwa ni kuwapo kwa kiwango mfuto (flat rate) vya kodi ya majengo na kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa mkusanyaji pekee wa kodi ya majengo.

“Viwango vinavyopendekezwa ni Sh20,000 kwa nyumba za ghorofa katika maeneo ya vijijini na Sh50,000 kwa kila sakafu kwa nyumba za ghorofa katika maeneo ya mjini,” alisema.

Awali, wamiliki wa majengo walikuwa wakikadiriwa kodi kutokana na thamani ya nyumba na mahali ilipojengwa.

Advertisement