Serikali yatafuta masoko mazao ya kilimo nje ya nchi

Tuesday November 27 2018

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema wizara yake imetuma watu kwenda kutafuta masoko ya mazao ya kilimo nje ya nchi ili kuwapatia wakulima taarifa sahihi za masoko kwa mazao yao.

Akizungumza kwenye warsha ya wadau wa kilimo iliyoandaliwa na Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) jana, Hasunga alisema msimu huu umekuwa na mavuno mazuri, hivyo Serikali imeamua kufungua mipaka ili wakulima wauze mazao yao popote.

“Tumefungua mipaka ili mtu auze mazao yake mahali popote. Pia, tumetuma watu kwenda kuangalia masoko nje ya nchi, kwenye nchi za Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Burundi,” alisema.

Waziri huyo alisema sekta ya kilimo nchini imekuwa mpaka kufikia asilimia 7.1 ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.9 uliokuwapo hapo kabla.

Kuhusu suala la korosho, alisema azma ya Serikali ni kununua korosho yote ya wakulima na kuhakikisha inabanguliwa hapa nchini.

Mwenyekiti wa bodi ya ACT, Dk Sinare Yusuph Sinare aliitaka Serikali kuongeza bajeti ya kilimo ili sekta hiyo ifanye vizuri. Alisema makubaliano yaliyofikiwa kwenye Azimio la Maputo yalikuwa ni kutenga asilimia 10 ya bajeti kwenye sekta ya kilimo.

“Bado kilimo chetu kiko nyuma, masoko ya mazao ni changamoto, mazao yameshuka bei kwa kiwango kikubwa. Tukiisimamia Commodity Stock Exchange itasaidia kuepusha kuporomoka kwa bei,” alisema Dk Sinare.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Denmark (Danida), Elizabeth Mushi alisema zaidi ya asilimia 40 ya msaada unaotolewa na shirika hilo unakwenda kwenye sekta ya kilimo, hivyo ni vema nguvu ikaelekezwa kwa vijana kushiriki kikamilifu kwenye sekta hiyo.

Mushi alisema mafunzo ni muhimu kwa wanafunzi na vijana ambao wamejiajiri kwenye sekta hiyo.

Alisema Serikali iweke mipango ya kuwafikia wakulima wengi ambao wanaishi vijijini ili kuwapatia elimu na mafunzo ya kilimo bora.


Advertisement