Serikali yatakiwa kutenga maeneo ya kilimo kwa vijana

Thursday February 14 2019

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali imetakiwa kutenga ekari 20 kwa kila kijiji kwa ajili ya shughuli za kilimo kwa vijana ili kuinua pato la nchi na uchumi wa viwanda.

Ushauri huo umetolea leo Alhamisi Februari 14, 2019 jijini  Dodoma na mkurugenzi msaidizi wa maendeleo ya uchumi wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (Usaid), Michelle Corzine kwenye kongamano la uwekezaji biashara kilimo kwa vijana.

Corzine amesema idadi ya vijana nchini Tanzania inaongeza kwa kasi hivyo bila ya kuwepo kwa mbinu mbadala ya kuwafanya wawe na kazi, maisha yao hayatakuwa mazuri.

Amesema ifikapo 2025 Tanzania inakadiriwa kuwa idadi ya vijana wenye miaka wa miaka 15- 35 watakuwa ni asilimia 35 ya Watanzania wote, kwamba kundi hilo ni kubwa linahitaji mbinu za kulisaidia.

Mkurugenzi huyo amesema ili kubadili uchumi kuelekea kipato cha kati, ni vyema kundi hilo likatazamwa kwa namba yake na kupewa fursa.

“Hata hivyo kuna changamoto ya upatikanaji wa miundo rasmi ya fedha suala linaloathiri vijana na wakina mama katika kuzifikia ndoto zao,” amesema

Amesema kilimo kama ilivyo kwa biashara nyingine yoyote, mtaji ni muhimu na hivyo vijana wanahitaji kujengewa uwezo wa kuhimili mikopo na riba kubwa ambazo hutolewa na taasisi za kifedha.

 


Advertisement