Serikali yatoa maelekezo mapya mifuko ya plastiki

Dodoma. Serikali imesema wafanyabiashara watakaokuwa na mifuko ya plastiki katika maghala yao hadi Juni Mosi na kutaka kuuza nje ya nchi watalazimika kupata kibali cha Ofisi ya Makamu ya Rais na watasindikizwa hadi mpakani.

Akizungumza na Mwananchi jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema wafanyabiashara watakaokuwa na mifuko hiyo katika maghala yao watatakiwa kubaki nayo hapo hapo.

“Baadaye utafanyika utaratibu wa kurejerezwa (recycle) na kutengenezwa bidhaa nyingine kama sahani, viti na kadhalika,” alisema.

Hata hivyo, alisema mfanyabiashara atakayepata soko nje ya nchi anaweza kuruhusiwa kuuza kwa kibali maalum.

“Kwa mfano Sudan hawajakataza mifuko, tutawasaidia wale waliopata soko wasipate hasara lakini kwa kibali maalum na itasindikizwa hadi mpakani kwa gharama za msafirishaji,” alisema.

Mifuko mbadala

Waziri huyo alisema viwanda 70 vimejitokeza kutengeneza mifuko mbadala, ambapo kati ya hivyo sita ni vikubwa na vya kati 30.

Akizungumza na wakuu wa mikoa mwanzoni mwa wiki hii, Makamba alisema kanuni za kupiga marufuku mifuko ya plastiki zitachapishwa katika gazeti la Serikali leo na kwamba zitatafsiriwa kwa lugha ya kiswahili.