VIDEO: Serikali yatoa tamko usajili mpya laini za simu

Dodoma. Wakati wananchi wakikuna vichwa kuhusu usajili mpya wa laini za simu kutokana na kutokuwa na vitambulisho vya uraia, Serikali imesema wasio na vitambulisho hivyo watawekewa utaratibu maalum.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola baada ya Mbunge Viti Maalum (CCM), Felista Bura kuomba wongozo na kuhoji kuhusu usajili huo na changamoto ya wananchi kutokuwa na vitambulisho vya uraia.

“Mtanzania huyu tutampa utaratibu kwa sababu si kosa lake kutosajiliwa simu kwa sababu Serikali tupo kwa ajili ya kuwalinda Watanzania,” amesema.

Lugola ametoa ufafanuzi huo baada ya awali majibu ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye kutowaridhisha wabunge wengi walioonekana kusimama kutaka maelezo zaidi.

 “Watanzania hawapaswi kuwa na maisha ya wasiwasi, lazima waendelee kutumia simu kuanzia anainunua mpaka pale atakapoacha kuitumia. Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) tulikuwa na lengo la kutambua na kutoa vitambulisho milioni 24.5, hayo ndiyo malengo.”

“Lakini mpaka sasa Nida tumekwishafanya utambuzi, usajili wa Watanzania wenye sifa milioni 16, tulipoona kwamba wenzetu wa TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania)  wanataka kubadilisha masuala ya kusajili simu ili waweze kutumia alama za vidole na kwamba mwenye kitambulisho cha taifa ndio atakayesajiliwa,sisi kupitia Nida tuliweka utaratibu.”

 “Watanzania  ambao wamekwishapata vitambulisho watatumia  vitambulisho vyao. Watanzania milioni 16 tayari wameshapatiwa namba inaitwa NIN yaani National Identification Number, kwa hiyo namba hiyo ambayo anasubiri apewe kitambulisho chake ndiyo atakayoiwasilisha NIDA,” amesema.

Lugola amesema namba hiyo itawasilishwa TCRA na mhusika ataitumia kusajiliwa. “Kwa hiyo maana yake kibindoni tuna Watanzania milioni 16 ambao wana sifa za kusajiliwa kwenye simu na mpaka sasa tunaendelea kumalizia wale waliobaki katika kuwapa namba na kuendelea kutoa vitambulisho.”

Katika mwongozo wake, Bura alisema baada ya Serikali kutangaza mpango huo wa usajili sharti likiwa lazima muhusika kuwa na kitambulisho cha uraia yameibuka malalamiko kwa watu wasiokuwa na vitambulisho hivyo.

“Kwa kuwa leo inasomwa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Nida (Mamlaka ya Usajili wa Vitambulisho vya Taifa) wapo hapa naomba Serikali itoe majibu kuhusu jambo hili,” alisema Bura.

Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge pia aliitaka Serikali kutoa ufafanuzi wa kina katika jambo hilo kwa maelezo kuwa kasi ya utoaji wa vitambulisho hivyo kwa sasa si kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

“Ni kweli kuanzia Mei Mosi mwaka huu kampuni zote za simu zinatakiwa kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole baada ya kujiridhisha na utambuzi wa mtu kupitia kitambulisho cha tafa,”  alisema Nditiye.

“Tulianza usajili huu kwa majaribio na sasa tunataka kulifanya rasmi zoezi hili baada ya kujiridhisha taratibu zote zipo sawa. Watu ambao wana namba za vitambulisho wapo milioni 16.”

Hata hivyo, Nditiye alisema litaanza Mei Mosi mwaka huu na watafanya tathmini Septemba mwaka huu na kwamba  litamalizika Desemba 31 mwaka huu.

“Baada ya hapo laini ambazo watu watakuwa hawajasajili zitazimwa,” alisema Nditiye na kuamsha zogo bungeni.