Serikali yawataka waliokashifiwa kwenda mahakamani

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe

Muktasari:

  • Serikali yazungumzia uhuru wa vyombo vya habari huku ikiwataka waliokashifiwa kwenda mahakamani kushtaki.

Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema habari yoyote inayochapishwa kumchafua mtu ni kashfa na kuwataka waliokashifiwa kufungua kesi mahakamani.

Dk Mwakyembe ameyasema hayo leo Jumanne, Aprili 22, 2019 wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Amesema anaweza kusimamisha magazeti anapoona masharti ya leseni yamekiukwa, wahusika hawaendi mahakamani badala yake wanakimbilia kwa mabalozi.

“Napata wapi mamlaka ya kulifungia gazeti. Na mimi namhoji Mheshimiwa Devota (Mbunge wa Viti Maalum- Chadema Devota Minja) ni kifungu kipi usipokubaliana na mkurugenzi kimbilia katika balozi, sijaona hicho kifungu?”Amehoji Dk Mwakyembe.

Dk Mwakyembe amesema hiyo ni aina fulani ya ulimbukeni maana sheria inamtaja waziri mwenye dhamana na kwamba usipokubaliana na maamuzi ya waziri, mlalamikaji anaweza kwenda mahakamani.

Amesema kuwa balozi zimekuwa zikifika ofisini kwake kuhusu suala hilo na kwamba wamekuwa wakiwauliza kama wamesoma hiyo sheria. Dk Mwakyembe amesema waziri ana mamlaka chini ya kifungu cha 59 cha sheria kuzuia uchapishaji wa maudhui yenye athari kwa usalama wa nchi na amani katika jamii na kwamba anafikia hatua hiyo baada ya mchapishaji kuonywa.

Amesema hatua hiyo inafuata baada ya gazeti kuonywa mara nyingi na kwamba wao hawawezi kuona kwa sababu hawafanyi kazi katika vyombo hivyo.

Amehoji wanataka dola ifanye nini kwa kuvunjiwa heshima na kwamba akifika kwao mlalamikaji kwa kifungu cha 40 wanachofanya ni kumtaka mlalamikiwa kuomba radhi na wengi wanafanya hivyo ama kwenda mahakamani.

Amewashauri wanaokashifiwa kuepuka kujichukulia hatua kwa kuwananga kupitia njia mbalimbali za mahusiano kwa kumnanga mlalamikiwa kwa sababu unaondoa uzito wa kesi zao wenyewe.

Naye Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amesema hawawezi kuacha kuonyesha ziara za Rais John Magufuli katika Televisheni ya TBC kwa kuwa TBC ni chombo cha umma na Rais Magufuli anafanya kazi ya Watanzania, hafanyi kazi ya chama na anagusa matatizo ya wanyonge.

“Mtakuwa mashahidi anapopita huko mikoani utakuta Watanzania wanafuatilia kazi ambazo anazifanya iwe kwenye mabaa, masaluni, hadi kwenye mabenki kwa sababu Watanzania wanatakiwa kuona namna gani mheshimiwa Rais anafanya kazi,” amesema.