Serikali yawatoa hofu wamiliki maduka ya kubadilisha fedha

Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alipowasili kufungua semina ya wanahisa wa benki hiyo jijini  Arusha jana. Wa pili kushoto ni Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA),Charles Kicheere na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB, Ally Laay. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Majaliwa alizishauri benki kutoa majibu yatakayokidhi hoja za wanahisa kuhusu uendeshaji unaofanywa na menejimenti.

Arusha. Baada ya kufungia maduka kadhaa ya kubadilishia fedha za kigeni, Serikali imewataka wamiliki kuwa watulivu kwa sababu baada ya muda mfupi ujao wataruhusiwa kuendelea na biashara hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akifungua semina ya wanahisa wa Benki ya CRDB ikiwa ni sehemu ya mkutano mkuu wa 24 za benki hiyo.

Serikali ilifanya ukaguzi wa kushtukiza katika maduka kadhaa ya mkoani Arusha, Kilimanjaro na dar es Salaam na mengi kufungwa kwa maelezo kuwa yalikuwa yakifanya kazi kinyume cha sheria. Maofisa wa Serikali walidaiwa kuchukua fedha na simu za wamiliki kwa maelezo kuwa watapewa taarifa baadaye.

Baada ya maduka mengi kufungwa, Benki Kuu (BoT) iliwataka wananchi kubadilisha fedha zao kwenye benki za biashara na taasisi za fedha pamoja na maduka ya Shirika la Posta Tanzania.

Lakini jana, Majaliwa alisema kinachofanywa ni juhudi za Serikali kuboresha mazingira ya utendaji wa taasisi za fedha ambao ni muhimu kufanikisha malengo ya kiuchumi.

Alisema mwaka jana, benki tano ambazo hazikuwa na mtaji wa kutosha zilifungwa ili kulinda uchumi usianguke na operesheni ya kukagua na kuyafunga maduka ya kubadilisha fedha ulikuwa ni mkakati wenye mrengo huo pia.

“Wamiliki wa maduka ya kubadili fedha yaliyofungwa wawe watulivu. Benki Kuu inakamilisha utaratibu kabla ya kuwaruhusu waendelee na biashara na kuwahudumia wateja wao,” alisema Majaliwa.

Majaliwa alisema ni muendelezo wa Serikali kuhamasisha uzingatiaji wa utawala bora kuanzia ofisi za umma hadi taasisi za fedha kama CRDB.

Alisema ili kuhakikisha kila mwenye dhamana anafuata misingi ya utawala bora, Serikali inahamasisha uwazi, uwajibiaji katika uendeshaji wa kampuni za umma na binafsi.

“CRDB bado ipo juu kutokana na misingi imara aliyoijenga (aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa CRDB) Dk Charles Kimei ambayo (mkurugenzi wa sasa, Abdulmajid) Nsekela unaiendeleza,” alisema Majaliwa.

Majaliwa alizishauri benki kutoa majibu yatakayokidhi hoja za wanahisa kuhusu uendeshaji unaofanywa na menejimenti.

Aliipongeza menejimenti ya benki hiyo kwa uwazi ilionao na ukiwamo uwakilishi mzuri kwenye bodi ya wakurugenzi ambako wanahisa wadogo zaidi ya 29,000 waliopo wanapewa nafasi ya kusikilizwa na kutoa maoni yao.

Kwa upande wake, mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema jiji hilo la kitalii linahitaji sana fedha za kigeni ambazo sasa zinapatika benki, lakini matawi mengi yaliyopo yanafungwa kati ya saa 9:00 alasiri na saa 12:00 jioni, hivyo huduma kutopatikana kwa baadhi ya wageni wenye uhitaji.

“Naiomba CRDB ianzishe walau tawi moja litakalokuwa linaendelea kutoa huduma mpaka saa 5:00 usiku. Vilevile, Serikali imetoa vitambulisho vya wamachinga, naiomba benki iandae utaratibu wa kuwatambua na kuwakopesha ili tuandae mabilionea wengine baada ya kifo cha mzee (Reginald) Mengi,” alisema Gambo.

Kabla ya kufunguliwa kwa semina hiyo, mkurugenzi mtendaji wa CRDB alisema tangu alipoteuliwa kuiongoza benki hiyo Oktoba mwaka jana, watu wengi walimueleza matarajio yao.

“Walisema uchumi imara wa Taifa unategemea benki imara. Leo tunatoa semina kwa wanahisa ili kuwaonyesha fursa zilizopo ndani ya benki na kwenye sekta ya viwanda ambayo Serikali inahamasisha,” alisema Nsekela.

Kwa fursa zitakazobainishwa na wanahisa, Nsekela alisema benki ipo tayari kuwakopesha mtaji ili kufanikisha miradi yao.