Serukamba alivyotikisa mitandaoni kwa michango yake miwili bungeni

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba amezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii tangu juzi usiku kutokana video zake zinazomuonyesha akichangia hoja katika la Bunge la bajeti la mwaka 2018/2019, na hili la 2019/2020 linaloendelea Dodoma.

Video iliyosambazwa kwa kasi katika mitandao hiyo, ni ile inayomuonyesha akichangia mjadala wa Bunge la bajeti la 2018/2019, mbunge huyo alikuwa akijadili juu ya deni la Taifa.

Video hiyo inamuonyesha Serukamba akisema kuwa Serikali inataka kufanya kila jambo yenyewe bila kushirikisha sekta binafsi. Lakini pia akisema kumekuwa na kasoro nyingi kwenye ukusanyaji wa kodi.

Mchango huo umeonekana kushabihiana kiasi na ule alioutoa Jumatatu iliyopita katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2019/2020 ambako aligusia pia sekta binafsi na kukwama kwa biashara kutokana na mifumo na taratibu zilizopo. Mara zote mbili alizozungumza, Serukamba alieleza kwa kina jinsi masuala mbalimbali yanavyokwamisha kukua kwa biashara na kilimo kinachofanywa kwa takribani asilimia 65 na Watanzania.

Katika mchango wake wa Jumatatu, Serukamba alisema, “Asilimia 97 ya kazi Tanzania zinatekelezwa na sekta binafsi. Kama kuna mwajiri wa kwanza mkubwa Tanzania ni sekta binafsi, lazima mwajiri huyu tumlinde, lazima tuje na utaratibu ili afanye vizuri zaidi.”

Alisema benki za maendeleo na biashara zilizopo nchini kazi yake ni kuchochea uchumi na biashara na kutaka benki hizo kuandaliwa mazingira rafiki ili watu wakope na kuwekeza ili biashara ichangamke.

“Leo umeanzisha biashara umekopa benki unakwenda kufanya biashara, ila ukishindwa kulipa deni benki inauza nyumba na TRA wanakuja na kusema kabla ya kuchukua hela zako benki huyu tunamdai kodi tupe kodi yetu na kinachotokea NPL (mikopo chechefu) inapanda.

“Leo TRA kwenye mikopo ya nyumba wana nguvu kuliko aliyetoa fedha, maana yake ni moja, watu wengi hawatakopeshwa kwenye benki, utakuta wanaokopeshwa ni wakubwa, wadogo inaanza kuwa shida. Kipaumble cha TRA kwa ajili ya mapato ni jambo zuri ila tufahamu bila taasisi za fedha, biashara haiwezi kuchangamka,” alisema.

Serukamba alihoji sababu za sekta ya kilimo kutokuwa wakati asilimia 80 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo, “sababu ya kwanza ni kuendelea kuwa na kilimo cha utamaduni badala ya kilimo cha biashara. Zimbabwe waliua kilimo cha biashara wanalia njaa hivi sasa.

“Tuna ardhi kubwa, lazima tuje na mkakati wa kukua tujiulize maswali kwenye kahawa, pamba, korosho tumekua? Pamoja na Tanzania kuwa na ardhi kubwa, tunazalisha tani 50,000 za kahawa, Uganda wanazalisha tani 288,000 kuna kitu hatujafanya. Tukifanya mabenki yafanye vizuri watakopesha wakulima, wafanyabiashara na kukua kwa biashara na kilimo.”

Alichosema 2018

Katika mchango wake wakati huo, Serukamba alisema, “deni la Taifa linapanda kwa Sh4 trilioni kwa mwaka kulingana na ripoti ya BoT (Benki Kuu ya Tanzania) maana yake tumeamua kila kitu kinafanywa na Serikali, hatuwezi kuendelea.”

Mbunge huyo alisema hakuna Taifa duniani ambalo kila kitu kinafanywa kwa fedha zake, kusisitiza kuwa hata kama ni mkopo bado unabaki kuwa wa Serikali husika.

“Mwenyekiti (wa Bunge) wewe shahidi uwanja wa ndege wa Moscow International umejengwa na mtu. Humu ndani tunasema tutafanya PPP (Sekta Umma na Sekta Binafsi) lakini ukitafuta miradi ya PPP haipo na Serikali hii haiamini katika sekta binafsi.

“Bunge hili tukubaliane, waziri wa fedha atuambie Serikali hii haikubaliani na sekta binafsi kwa sababu mipango yako mwanzo mpaka mwisho huongelei sekta binafsi, kama tumerudi katika ujamaa tuambie tujue, lakini haiwezekani tuimbe ujamaa na kutaka matokeo ya kibepari,” alisema Serukamba.

“Ninamuonea huruma sana Rais (John Magufuli) anahangaika ila wenzake hawamuelezi ukweli mtanisamehe. Leo Rais anasema viwanda vizalishe sukari lakini tumesema siku zote bungeni hakuna aliyetuelewa ila kwa kuwa Rais kasema, viwanda vitazalisha sasa.”